Home Siasa MGOMBEA URAIS ATINGA KUCHUKUA FOMU NA USAFIRI WA BAJAJI

MGOMBEA URAIS ATINGA KUCHUKUA FOMU NA USAFIRI WA BAJAJI

0

………………………………………………………………….

Na Alex Sonna,Dodoma
Mgombea Urais wa Chama cha Demokrasia Makini, Sesilia Mmanga ametinga katika Ofisi yaTume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC), kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwania nafasi hiyo akitumia usafiri wa bajaji.

Mmanga amefika katika ofisi hiyo akiwa ameambatana na Mgombea Mwenza wake Tabu Musa Juma na wanachama wengine kwa usafiri huo kukabidhiwa fomu na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu, Mmanga amesema wananchi na wakulima wa hali ya chini usafiri wao ni wa bajaji na kwenye kampeni za uchaguzi watatumia usafiri huo pamoja na pikipiki, baiskeli, guta na punda.

“Maana ya Makini ni Maarifa, Kilimo na Nishati, tumekuja na usafiri wa bajaji na bodaboda ili kuudhihirishia umma watakaponiteua mimi kama mama, wengi wananiita mama ushauri au mama THT, mama wa vipaji, hatutawabagua hata wale wa hali ya chini, tumekuja kivingine ili kuleta mabadiliko,”amesema.

Mmanga amesema katika kampeni zao watatumia usafiri huo pamoja na guta, baiskeli na punda kwa kuwa wakulima wengi wanatumia baiskeli na punda ndo mbeba mizigo.
“Wakulima ni wengi tumejipanga, hatutalala kwa kuwa ukilala nchi inauzwa na sisi hatutaki nchi iiuzwe,”amesema.