UONGOZI wa Yanga SC umetangaza rasmi kuachana na mabeki wake wakongwe, Juma Abdul Jaffar Mnyamani na Kelvin Patrick Yondan baada ya kushindwa kufikia nao makubaliano ya kusaini mikataba mipya.
Taarifa ya Yanga SC jioni ya leo imesema; “Uongozi wa Mabingwa wa Kihistoria nchini, leo unatangaza rasmi kuachana na wachezaji wake Nyota, Kelvin Yondani na Juma Abdul baada ya kushindwa kufikia makubaliano,”.
Abdul na Yondan wanafanya idadi ya wachezaji walioachwa Yanga SC kufika 16, baada ya wengine 14 kutemwa mwanzoni mwa wiki.
Hao ni mabeki, Jaffary Mohamed, Andrew Vincent ‘Dante’, viungo Mohamed Issa ‘Banka’ na Mrisho Ngassa wote wazawa, aliyekuwa Nahodha, Papy Kabamba Tshishimbi, washambuliaji David Molinga ‘Falcao’ wote kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Tariq Seif, mzawa pia ambao nao pia wamemaliza mikataba.
Wengine ni Ally Mtoni ‘Sonso’, Muharami Issa ‘Marcelo’, Ali Ali, viungo Mnyarwanda Patrick Sibomana, Mzambia Erick Kabamba, Rapahael Daudi na mshambuliaji Muivory Coast, Yikpe Gislain ambao wao wamesitishiwa mikataba.
Wachezaji 15 tu kutoka kikosi cha msimu uliopita wamepitishwa kubaki ambao ni makipa Mkenya Farouk Shikhalo, Metacha Mnata na Ramadhan Kabwili na mabeki Paul Godfrey ‘Boxer’ na Mghana, Lamine Moro.
Wengne ni viungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima, Mghana Bernard Morrison, Feisal Salum, Juma Mahadhi, Adeyoum Ahmed, Said Juma ‘Makapu’, Balama Mapinduzi, Deus Kaseke, Ditram Nchimbi na Abdulaziz Makame.
Tayari Yanga SC imesajili wachezaji watano wapya, ambao ni mabeki Yassin Mustapha kutoka Polisi Tanzana ya Kilimanjaro, Bakari Mwamnyeto kutoka Coastal Union ya Tanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ aliyerejeshwa baada ya msimu mmoja wa kucheza Marekani, kiungo Zawadi Mauya kutoka Kagera Sugar na mshambuliaji Waziri Junior kutoka Mbao FC ya Mwanza iliyoshuka Daraja.