…………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Watanzania wametakiwa kujenga utamaduni wa ulaji wa nyama kwani takwimu zinaonyesha kiwango cha ulaji wa nyama kiko chini ambapo sasa ulaji umefikia asilimia 15 huku Shirika la Afya Duniani likitaja Mtu wa kawaida anatakiwa kula angalau kilo 50 kwa mwaka.
Akizungumza Jijini Dodoma kwenye paredi ya mifugo kwenye maonesho ya mifugo na wakulima nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo Profesa Elisante Ole Gabriel amesema kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa Tanzania bado ulaji sio mzuri ambapo takwimu zinaonesha mwaka 2017/ 18 ulaji wa nyama ulikuwa kilo 10 kwa mwaka.
“Angalau kiwango kimekuwa kidogo sasa tumefikisha kilo 15 mwaka, bado tuko chini sana .Watanzania wajitahidi kula nyama ambayo ni sahihi,” amesema Ole Gabriel.
Aidha amesema kwa kiwango sasa unywaji wa maziwa umefikia lita 200 kwa mwaka, lakini mwaka 2018/19 unywaji wa maziwa ulikuwa lita 54 kwa mwaka kama Wizara wanaendelea kuhamasisha Watanzania kuendelea kunywa maziwa kwa wingi.
Profesa Gabriel amesema watatoa kipaumbele kuhakikisha ubora wa mifugo unaendelea kuwa bora na kuachana na ufugaji wa mazoea bali watu wafuge kwa tija.
Amesema katika kipindi cha Serikali ya awamu ya tano katika sekta ya mifugo kuna mambo mawili yametokea.
“Wakati Rais John Magufuli akiingia madarakani Wizara hiyo ilikuwa ikichangia bilioni 14 lakini imeongezeka hadi kufikia bilioni 44.5 ni sawa na ongezeko la asilimia Zaidi ya 200″.
“Pia mifugo imeongezeka sasa kuna ng’ombe milioni 33, mbuzi milioni 23, kondoo zaidi ya milioni sita, kuku milioni 83 na kuku mayai yamefika bilioni nne.
“Mayai peke yake ni bilioni 800 hii ni jambo kubwa sana, lazima juhudi ziongezwe.,” amesema.
Amesema uchakataji wa kuongeza thamani kwenye ngozi ni jambo la msingi Watanzania wapende kutumia bidhaa za ngozi zilizotengenezwa hapa hapa nchini.
Hadi mwaka jana jozi za viatu zilizotengenezwa kwa ngozi zilikuwa ni 1.2 kwa mwaka, idadi hiyo ni ndogo kulinganisha na ngozi zinazozalishwa hapa nchini.
“Endapo kina mama wote watanunua pochi na kuvaa viatu vya ngozi zetu hilo litakuwa jambo jema sana, tutaendelea kujipanga kuboresha tunayoyafanya,” amesema.
Kwa upande wake, mgeni rasmi katika maonesho hayo ambaye ni Kaimu mkuu wa mkoa wa Dodoma ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda amesema sekta ya mifugo ikisimamiwa vizuri itachangia fedha za kutosha katika pato la taifa.
Aidha amesema katika maonesho ya mifugo yanaonesha ni kiasi gani mifugo ikifugwa vizuri inaweza kubadilisha maisha ya wakulima na wafugaji na kufaidika na kazi zao.
“Huwezi kuamini ng’ombe kama hawa wapo kama Kongwa, Mpwapwa na Chemba na mnasema Dodoma ina ukame sasa hawa ng’ombe mbona wana zaidi ya kilo 900, lazima kitu kifanyike hapa,” amesema.
Amebainisha kuwa kwa wilaya ya Bahi asilimia 80 ya makusanyo ya ndani yanatokana na mifugo unaweza kuona halmashauri inategemea mifugo unaweza kuwa na maono mazuri ya maonesho ya mifugo.
Nae Katibu tawala Mkoa wa Singida Angelina Lutambi amesema, maonesho hayo yamekuwa ni elimu kubwa sana kwa wananchi na watendaji wa ngazi mbalimbali za serikali na yamekuwa njia nzuri ya kujifunza.
Mkoa wa Singida uchumi wake unategemea kilimo na sekta ya mifuko ikiwa na idadi ya mifugo zaidi ya milioni 1.3 lakini shughuli hizo zikifanyika kitaalam wananchi watakuwa na uchumi mkubwa katika familia.