Dodoma,
Tanzania imesaini Mkataba wa mapitio wa Georgetown unaosimamia mahusiano na uendeshaji wa Jumuiya ya Nchi za
Afrika, Caribiani na Pasifiki ambayo zamani ilikuwa ikiitwa ACP na sasa Organisation of African,
Carribean and Pacific States (OACPS) iliyo
na nchi wanachama 79.
Mkataba huo ulisainiwa na balozi wa Tanzania nchini
Ubelgiji, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga kwa
niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Brussels, Ubelgiji
tarehe 31 Julai 2020. Hivyo Tanzania inakuwa nchi ya 42 kati ya nchi 79 kusaini
Mkataba wa mapitio wa Georgetown.
Mkataba
wa Georgetown umefanyiwa mapitio ili uweze kuendana na wakati kwa kuzingatia
mabadiliko makubwa yanayoendelea kutokea duniani katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimazingira
tangu kuanzishwa kwa ACP mwaka 1975. Mchakato wa kufanya mapitio ya mkataba huu
ulianza mwezi Machi 2013 kupitia timu maalum iliyoanzishwa kukusanya maoni na
kuleta mapendekezo chini ya Uenyekiti wa Rais Mstaafu wa Nigeria, Mhe. Olusegun Obasanjo.
Aidha,
Mwaka 2019 mchakato wa mapitio hayo ulihitimishwa kwa kuridhiwa na Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi
za OACPS katika mkutano wao
uliofanyika mwezi
Desemba 2019 jijini Nairobi, Kenya.
Mkataba wa Georgetown ndiyo ulianzisha ACP mwaka 1975 katika mji wa
Georgetown nchini Guyana. Tanzania
ilisaini Mkataba huo wa awali tarehe 11 Desemba 1975 na imedumu ikiwa
mwanachama wa ACP tangu wakati huo.
Pamoja
na kuwa mwanachama Tanzania imekuwa ikinufaika katika masuala ya kiuchumi,
kijamii, biashara, na uwekezaji kupitia ushirikiano maalum baina ya nchi za ACP
na Umoja wa Ulaya unaosimamiwa na mikataba ya Lome na Cotonou. Vilevile miradi ya ubia wa maendeleo
na ile ya mtangamano wa nchi za ACP chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo wa
Ulaya. Pia ushirikiano katika masuala ya kubadilishana ujuzi na uzoefu na nchi
za ACP, mshikamano wa kisiasa na kidiplomasia katika kutetea maslahi ya
Tanzania kimataifa kupitia jukwaa la ACP.
Imetolewa
na;
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali
======================================================
Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga akisaini Mkataba wa Mapitio wa Georgetown mjini Brussels – Ubelgiji tarehe 31 Julai, 2020.
Mhe. Nyamanga (katikati), Maafisa wa Ubalozi, na Mwanasheria wa Jumuiya ya OACPS, Dr Emmanuel
Opoku wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukamilisha zoezi la utiaji saini Mkataba huo.