Mwenza katika Uchaguzi Mkuu Mhe Samia Suluhu Hassan wakionesha fomu za
udhamini kwa wanachama wa CCM wa Dodoma baada ya kutoka kuchukua fomu
hizo za kugombea Urais
akiongea na wanachama wa CCM wa Dodoma baada ya kutoka kuchukua fomu
hizo za kugombea Urais kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi leo jijini Dodoma
Na. Alex Sonna, Dodoma
MwenyeKiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Dkt. John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mpeperusha bendera ya Mgombea Urais CCM leo amechukua Fomu za kugombea ili kutetea kiti chake cha Urais.
Akizungumza katika viwanja vya CCM White House,Dkt.Magufuli ameeleza kuwa ameamua kuchukua fomu yeye na Mgombea Mwenza Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi kingine cha miaka mitano ili kukamilisha miradi mingi ya maendeleo waliyoianza kwa awamu yao ya kwanza .
Aidha Dkt. Magufuli ameeleza kuwa wamefanya mambo mengi katika kipindi hiki,wamejenga shule za msingi Zaidi ya 908,shule za sekondari Zaidi ya 228 ,vituo vya afya Zaidi ya 500,mambo mengine mengi.
“Ukiangalia Dodoma tu ,tumefanya upanuzi wa uwanja wa ndege ,tumweka taa za barabarani,majengo mengi yamejengwa ,kuna program ya kujenga barabara ya njia nne yenye urefu wa kilometa 110 ambayo imetengewa Zaidi ya shilingi bilioni 700,uwanja wa ndege wa Msalato umetengewa shilingi milioni 600,fedha hizi zipo”, amesema Dkt. Magufuli.
“Hivyo nikiangalia sioni mwingine wa kuja kuyafanya hayo ,tunajenga reli ya mwendokasi ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 87 kwa kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na kpande cha Morogoro-Dodoma ujenzi wake umefikia asilimia 32 na tunahitaji tuendelee mpaka Mwanza,nikiacha,yataachiwa pale ,ndio maana nimeona tugombee tena na Mama Samia.”amesisitiza Dkt. Magufuli.
Katika hatua nyingine Dkt. Magufuli ameeleza kuwa katika kipndi chake cha miaka mitano umeme umesambazwa katika vijiji 9,402 kutoka vijiji 3,000 wakati tunaingia madarakani ,vimebaki vijiji 3,000 ambavyo alisema havitamshinda kuvifikia kwa miaka mitano.
Naye Mgombea Mwenza wa Dkt. Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia amempongeza Rais Magufuli kwa kuhakikisha vifo vya akina mama na Watoto kupungua kutokana na ujenzi wa vituo vya afya nchini lakini pia amepunguza tatizo la upatikanaji wa maji ambapo sasa yanapatikana kwa asilimia 74 na kutoa elimu bila malipo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu CCM Dkt.Bashiru Ally chama hicho kimewasha mitambo yake rasmi huku akitoa majukumu kwa jumuiya za chama hicho.
“Mitambo ya kuhakikisha CCM inashinda imewashwa rasmi leo,muda wa kutesti mitambo umeisha , sasa ni kazi ya kulinda kura,kuhamasisha wapiga kura nyumba kwa nyumba ,kitanda kwa kitanda kwenda kupiga kura,na jukumu hili nalikabidhi kwa UVCCM,
Dkt. Bashiru ameeleza kuwa Mitambo hii ya kisasa inahitaji Mafuta,ikiishiwa maji inahitaji maji ya kupoozea,jukumu hilo amemkabidhi kwa UWT na mwendeshaji wa mitambo hii ni Jumuiya ya Wazazi.
“Kwa hiyo nakuhakikishia Mwenyekiti safari ushindi utakuwa ni wa kishindo kikubwa ,udiwani tutaongoza Halmashauri zote nchi nzima ,tutakuwa na wabunge wengi kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi ,na urais Zanzibar tutashinda mchana mapema.”amesisitiza Dkt. Bashiru.