Na Mwandishi Wetu, Morogoro
MAMLAKA ya Hali ya Hewa (TMA) imesema wakulima wanaotumia taarifa za hali ya hewa zimekuwa na tija na msaada mkubwa kwenye shughuli zao. Hii ni kutokana na ukweli kwamba taarifa za hali ya hewa ni msaada mkubwa kwenye maendeleo ya uchumi wa nchi, mkulima mmoja mmoja na mwananchi yeyote kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Mtaalam wa Hali ya Hewa nchini Tanzania, Dk. Alfred Kandowe alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika Morogoro.
Alisema, TMA kwa sasa ina mfumo maalumu wa utoaji taarifa za hali ya hewa kwa wananchi wenye simu za kawaida kabisa (zisizo simu janja) kupitia meseji za kawaida ujulikanao kama ‘farm sms’ ambao usambaza taarifa kwa wakulima, wafugaji na wavuvi waliojiunga na kujiunga ni rahisi kabisa.
Aliongeza taarifa hii humfikia mteja wetu kila tunapozituma kuanzia taarifa za hali ya hewa za ndani ya siku 10, za mwezi na hadi zile tunazozitoa kwa muda mrefu, akielezea namna ya mkulima kujiunga alisema; “Ili mteja wetu yeyote aweze kujiunga kwenye mfumo huu wa kupata taarifa za hali ya hewa kupitia simu za kiganjani, kuna fomu zetu ambazo kila tunapopita huwa tunawapa wateja na hata wadau wetu wanajaza taarifa zao…na taarifa ya msingi ni namba ya simu ya mteja ambayo itapokea meseji, anataka kupata taarifa kwenye eneo gani na akitaja tunamtengenezea eneo husika na kumtumia..,”
Aidha aliongeza kuwa utoaji wa taarifa zetu za hali ya hewa umeboreshwa hivyo mteja anaweza kupata taarifa hizo kwa eneo lake tu na hata kwa muda fulani, kulingana na mahitaji ya mteja wetu. “…Mkulima, mfugaji au mvuvi yeyote akitaka taarifa kwa eneo lake tu tunaweza kumtumia kulingana na mahitaji yake, na atazipokea moja kwa moja kwenye namba ya simu aliyotupatia,” alisema Ofisa huyo.
Pamoja na mambo mengine TMA, wamejipanga kuelimisha wateja wetu, kwamba namna gani wanaweza kupata elimu na taarifa za hali ya hewatu kuanzia namna tunazitafuta, kuzichakata na hadi zinamfikia mteja wetu yaani mwananchi. Wakulima, wafugaji na wavuvi wanaweza kupata taarifa hizi kupitia vyombo mbalimbali zikiwemo redio, televisheni na kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kupitia simu janja.
Banda la Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania, kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika Morogoro. |