Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na baadhi ya viongozi wa Chuo hicho wakipata picha ya pamoja na baadhi ya Wahitimu wa Chuo hicho katika Mahafali ya 50 ya digrii ya Uzamili.Wahitimu wa Chuo hicho katika Mahafali ya 50 ya digrii ya Uzamili wakiwa kwenye maandamo kuelekea ukumbi wa Nkuruma kwaajili ya sherehe ya 50 ya Kutunuku Digrii za Uzamili.
**********************************
NA EMMANUEL MBATILO
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Prof.William Anangisye amewataka wahitimu wawe watu wa kutafuta fursa badala ya kusubiri fursa ziwafuate.
Akizungumza katika Sherehe ya 50 ya Kutunuku Digrii za Uzamili na Awali katika Ukumbi wa Nkuruma Jijini Dar es Salaam amewataka wahitimu wasikate tamaa hata pale watakaposhindwa kufikia mafanikio waliyotarajia bali waendelee kuwa na ari ya kujaribu tena na tena hadi mafanikio yapatikane.
“Mtakapokuwa mnatekeleza wajibu wenu wa kujitafutia maisha mazuri na kuendeleza nchi yetu, muwe na hulka ya kuthubutu kujaribu mambo ambayo yanaonekana ni magumu”. Amesema Prof.Anangisye.
Aidha Prof.Anangisye amesema tangu mahafali ya kwanza yq Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyofanyika mwaka 1970 Chuo kimeendelea kupata mafanikio makubwa , kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya wahitimu na program.
“Katika mahafali ya kwanza ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1970 kulikuwa na programu 10 na jumla ya wahitimu 485”. Amesema Prof.Anangisye.
Hivyo amesema kuwa idadi ya programu na Wahitimu iliongezeka tena kufikia programu 132 na wahitimu 6,830 mwaka 2010.
“Katika mahafali haya ya 50 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, duru ya kwanza, tunawahushurisha jumla ya wqhitimu 581 kati yao 47 wamefuzu na wanastahili kutunukiwa shahasa ya uzamivu, 465 wanastahili kutunukiwa shahada za umahiri, 18 wanastahili kutunukiwa stashahada ya uzamili na 51 wanastahili kutunukiwa shahada za awali”. Amesema
Nae Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Jaji Mstaafu, Mhe.Damian Lubuva amesema katika kukisimamia Chuo na kuboresha utendaji, kwa kuanzia kipindi cha mwezi Desemba 2019 hadi sasa.Baraza limeidhinisha sera na mapendekezo mbalimbali ikiwemo Pendekezo la mabadiliko ya Taasisi ya Usimamizi wa Rasilimali za Madini kuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo Baraza liliidhinisha ombi la Wizara ya Madini la Chuo hicho kuchukua usimamizi wa Chuo cha Madini ambacho hapo awali kilikuwa chini ya Wizara hiyo.
Aidha Mhe.Lubuva amesema Baraza la Chuo linatambua changamoto mbalimbali ambazo wafanyakazi wa chuo na wanafunzi wanakabiliana nazo na linaendelea na juhudi za kuzishughulikia.