Mkuu wa wilaya ya Kilolo, Asia Abdala akizungumza na wanahabari
…………………………………………………………………….
N A DENIS MLOWE, IRINGA
WAAJIRI wametakiwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 na kanuni zake za 2017 inayolinda, kuhimiza na kuendeleza unyonyeshaji watoto maziwa ya mama.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdalah kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Iringa, Ally Hapi wakati wa mkutano na wanahabari juu ya wiki ya Unyonyeshaji iliyoanza Agosti 1 hadi kilele chake Agosti 7 juu ya waajiri kuzingatia sheria hiyo kwa wanawake wote walioajiriwa katika sekta rasmi wapewe haki yao ya likizo ya uzazi kwa mujibu wa sheria waweze kunyonyesha
Asia Abdalah alisema kuwa licha waajiri kuzingatia sheria hiyo aidha jamii inapaswa kutoa kipaumbele cha kulinda haki za uzazi za wanawake waliojiriwa katika sekta isiyokuwa rasmi.
Alisema kuwa pamoja na juhudi zilizofanyika kwa lengo la kujenga mazingira wezeshi kwa wanawake wanaonyonyesha bado kumekuwepo changamoto mbalimbali zinazochangia kupunguza kasi ya unyonyeshaji katika jamii. Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na baadhi ya wanawake kushindwa kuwanyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo baada ya mtoto kuzaliwa.
Aliongeza kuwa licha ya changamoto ya baadhi ya waajiri kushindwa kufata sheria hiyo changamoto nyingine ni kazi nyingi zinazowakabili wanawake katika familia na jamii hivyo kukosa muda wa kupumzika na kunyonyesha watoto wao.
Alisema kuwa Mila na desturi za jamii kuhusu kuwaanzishia watoto wachanga vyakula vya nyongeza mapema kabla hawajatimiza umri wa miezi sita kama inavyopendekezwa na wataalamu wa afya ni changamoto nyingine ambayo wanayokabiliana nayo baadhi ya wanawake kwenye kunyonyesha.
Alisema kuwa mapendekezo ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuhusu taratibu zinazofaa za ulishaji wa watoto wachanga na wadogo ni kunyonyeshwa maziwa ya mama katika saa moja ya kwanza baada ya kuzaliwa ili kumkinga na tatizo la manjano, kufanya maziwa yaanze kutengenezwa mapema na yasikatike.
Aidha alisema kuwa Mtoto kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo na kuwakumbusha kuwa Mtoto kuanzishiwa chakula cha nyongeza anapotimiza umri wa miezi sita na kuendelea kunyonyeshwa hadi atimize umri wa miaka miwili au zaidi.
Alisema kuwa kama serikali inawajengea uwezo watoa huduma za afya na wanasihi na kuwataka Watoa huduma za afya na wanasihi rika waliopata mafunzo waliopo katika jamii wanahitaji kutoa huduma bora za lishe ya mama na mtoto.
“Miongoni mwa maeneo wanayohitaji kusisitiza ni suala zima la unasihi, elimu ya unyonyeshaji pamoja na stadi za kuwasaidia wanawake waweze kunyonyesha kwa ufanisi na kupewa elimu sahihi kuhusu ya unyonyeshaji. Elimu hii itawasaidia kukabiliana changamoto mbalimbali na Imani potofu zinazoathiri unyonyeshaji katika jamii” alisema
Aliongeza kuwa wanaimarisha Huduma za Mpango Rafiki wa Hospitali kwa Mama na Mtoto kwa Hospitali, vituo vya afya, zahanati na vituo vyote vinavyotoa huduma za uzazi zinapaswa kuzingatia vipengele kumi vya kufanikisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama.
Alivitaja miongoni mwa vipengele hivyo ni kutoa elimu ya lishe na unyonyeshaji kwa wanawake wote wajawazito wanaohudhuria kliniki ya afya ya uzazi, kuwasaidia wanawake wanaojifungua kuanza kunyonyesha watoto wao maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kujifungua, na kuwahimiza waendelee kunyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo.
Kilele cha siku ya onyeshaji mkoa inatarajiwa kufanyika wilaya ya Mufindi ikiambatana na kauli mbiu ya “Tuwawezeshe wanawake kunyonyesha watoto kwa afya bora na ulinzi wa mazingira”