***************************
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
SERIKALI mkoani Pwani imetekeleza agizo la Rais Dk John Magufuli la kufanyia matengenezo gari la wagonjwa la wilaya ya Rufiji ,ndani ya siku nne baada ya Rais kupita wilayani humo akitokea mkoani Mtwara kwenye mazishi ya aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu Benjamini Mkapa ambapo alipewa malalamiko na wananchi kuwa gari hilo halitoi huduma .
Ikumbukwe Rais Magufuli baada ya malalamiko hayo alitoa maelekezo kwa wilaya kutatua changamoto ya gari hilo la wagonjwa ndani ya siku tano liwe limekamilika na kuanza kazi ya kuhudumia wananchi.
Akizungumza mjini Kibaha mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo wakati akimkabidhi gari hilo,Mganga mkuu wa mkoa huo Gunini Kamba baada ya ukarabati alisema ,gari hilo lilipelekwa Temesa kwa ajili ya matengenezo.
Ndikilo alisema kuwa limekarabatiwa na leo siku ya nne liko tayari na linakabidhiwa kwa mganga mkuu wa mkoa Gunini Kamba naye anawakabidhi wananchi wa Rufiji kwa ajili ya kwenda kutoa huduma.
Aidha aliwataka waganga wakuu wa wilaya za mkoa huo kutengeneza magari ya wagonjwa ,wasisubiri kukumbushwa wajibu wao .
Ndikilo alieleza mkuu wa wilaya na mkurugenzi Rufiji lazima wasimamie kusitokee matatizo kama hayo yaliyotokea wilaya ya Rufiji.
“Tunashukuru kuwa tumetekeleza agizo la Rais la kutaka gari hilo la wagonjwa kuwa tayari ndani ya siku tano lakini sisi kabla ya siku moja iliyotakiwa kukamilika tayari tumeshakamilisha ukarabati na sasa inakwenda Rufiji kwa ajili ya kuanza kazi,”alisema Ndikilo.
Katika hatua nyingine alisema kuwa tayari matundu tisa yako kwenye hatua ya linta ambapo ujenzi wa vyoo saba na mabafu mawili ndivyo vinajengwa kwa ajili ya soko la Wilaya ya Kibiti na ujenzi umefikia zaidi ya asilimia 65.
Akizungumzia suala la Mkuranga ambapo Rais alitoa agizo la kutaka mgogoro wa ardhi kwenye eneo lenye ukubwa wa hekari 1,750 utatuliwe kwa kuwataka mkuu wa wilaya, mkurugenzi na mbunge na wizara ya ardhi watatue tatizo hilo.
Alisema wizara ya ardhi imewaita wahusika wote wa ardhi ile na wanafanya mazungumzo na kamishna wa ardhi na katibu mkuu wa ardhi na Waziri wa ardhi na maendeleo ya makazi William Lukuvi atakuwa na ziara mkoani Pwani na atatembelea eneo hilo.
Aliwataka wananchi waliovamia na kugawana eneo hilo waliachie na waziri atafika hapo ili kutatua mgogoro huo ili kila upande upate haki yake na kuondoa changamoto iliyojitokeza kwenye eneo hilo.