…………………………………………………………………………….
Na John Walter-Babati
Mwanafunzi Aisha Kilangwe (6) aliekuwa anasoma darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Sinai mjini Babati, amefariki dunia baada ya kugongwa na gari wakati akivuka kwenye kivuko cha watembea kwa miguu (Zebra) kuelekea shuleni mita chache kutoka bara bara kuu ya Babati-Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara Paul Kasabago amesema tukio hilo lilitokea tarehe 03/08/2020 majira ya saa nne asubuhi katika maeneo ya Sinai mtaa wa Maisaka kata ya Maisaka ambapo gari lenye namba za usajili T.873 BMX aina ya Mitsubishi Fuso basi linalofanya safari zake kutoka Bashnet kwenda Babati lilimgonga mwanafunzi huyo na kufariki dunia papo hapo baada ya kukanywagwa na tairi kichwani.
Kamanda Kasabago alisema tayari wameshamkamata dereva wa basi hilo John Gregory ambaye awali alitoroka mara baada ya ajali hiyo kutokea.
Kasabago ameeleza kuwa chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa dereva na kutozingatia alama za barabarani.
Aidha amewataka madereva na watumiaji wa vyombo vya moto kuwa makini wanapokuwa barabarani kuheshimu alama za barabarani ili kuepukana na ajali zinazoweza kuzuilika.