……………………………………………………………………………………………….
Na Mbaraka Kambona, Tabora
Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Masoko, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Felix Nandonde amewahimiza wafugaji nchini kufanya ufugaji wa kisasa, wenye tija na kuachana na ufugaji wa kienyeji ambao tija yake ni ndogo.
Dkt. Nandonde aliyasema hayo katika uzinduzi wa zoezi la kuhamasisha upandikizaji wa mbegu bora kwa ng’ombe jike lililofanyika katika Wilaya ya Uyuhi, Mkoani Tabora Mwishoni mwa wiki (Julai 30, 2020).
Akiongea baada ya kuzinduliwa kwa zoezi hilo ambalo linategemewa kufanyika nchi nzima, Dkt. Nandonde alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetenga kiasi cha shilingi milioni 145 kwa ajili ya kuhamasisha wafugaji kuboresha mifugo yao kwa kufanya ufugaji wa kisasa ikiwemo kutumia mbegu bora za mifugo.
“Mkakati wa Wizara kwa mwaka huu wa fedha (2020/ 2021) ni kufanya upandikizaji wa mbegu bora kwa ng’ombe jike milioni tatu (3) ili tuweze kupata ndama bora walau milioni moja,”alisema Dkt. Nandonde
“Lengo la zoezi hili ni kuwahamasisha wafugaji kufanya ufugaji wa kisasa ili wawe na ng’ombe bora watakaowawezesha kujiongezea kipato na kuboresha maisha ya mtu mmoja mmoja na kaya,”aliongeza Dkt. Nandonde
Aidha, Dkt. Nandonde alisema kuwa ili wafugaji waweze kuwa na mifugo bora ni muhimu sasa kuachana na ufugaji wa kienyeji na kufanya ufugaji wa kisasa kwa kuzingatia kuwa na malisho bora kwa ajili ya mifugo yao, kuzingatia chanjo za mifugo ili kuwalinda na magonjwa na eneo bora la kufugia.
“Serikali ya awamu ya tano imehamasisha ujenzi wa viwanda vya nyama hivyo hii ni fursa nzuri kwa wafugaji kuitumia katika kuboresha kipato chao kwa kuwa na mifugo bora itakayowapatia mazao bora kwa ajili ya kupeleka katika viwanda hivyo na kujipatia kipato cha uhakika,”alifafanua Dkt. Nandonde
Naye, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Msalika Makungu alisema kuwa zoezi hilo la kupandikiza mbegu bora litaleta tija kubwa kwa wafugaji kwa sababu litawafanya wawe na mifugo bora itakayowaongezea kipato chao binafsi na hata Mkoa.
“Mabadiliko ya tabia nchi yanayoendelea kutokea hayatoi fursa tena kwa ufugaji wa kienyeji, njia pekee itakayowafanya wafugaji waendelee kubaki katika sekta hiyo ni ufugaji wa kisasa, waachane na mtindo wa kuwa na kundi kubwa la mifugo na wawe na kundi dogo lenye tija kubwa,”alisema Makungu
Mwisho.