Nahodha wa Timu ya Tunduru Korosho FC ya Tunduru mkoani Ruvuma Tariq Seif kushoto, akimpa zawadi ya jezi mpya ya Timu hiyo Mkuu wa wilaya na mlezi wa Timu hiyi Julius Mtitiro mara baada ya Timu kuwasili wilayani humo ikitokea mkoani Kigoma kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa ngazi ya mikoa ambapo ilibuka Bingwa wa mashindano hayo.
PICHA na Mpiga Picha Wetu
……………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu,Tunduru
MKUU wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro amewataka wachezaji wa Timu ya Tunduru Korosho kutobweteka na mafanikio waliyoyapata, badala yake waongeze bidi ya mazoezi ili wafanye vizuri katika mashindano ya Ligi daraja la Pili Taifa.
Mtatiro ametoa kauli hiyo jana wakati wa mapokezi ya Timu hiyo katika viwanja vya Baraza la Idd Mjini Tunduru yaliyohudhuriwa na mamia ya wakazi wa mji wa Tunduru mara baada ya Timu hiyo kuwasili ikitokea Kigoma katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa.
Mtatiro ambaye ni mlezi wa Timu ya Tunduru Korosho alisema, baada ya kuwa mabingwa wa Ligi ya mabingwa wa mikoa, Timu hiyo inahitaji maandalizi ya uhakika sana ili kujiweka fiti kwa ushiriki wa ligi daraja la pili Taifa ambapo itakutana na Timu nyingine zenye uwezo mkubwa.
Aidha mlezi huyo amehaidi kuboresha maslahi ya wachezaji,benchi la ufundi pamoja na timu mzima kwa kulipa mishahara fedha zitakazotokana na michango ya wananchi wa Tunduru hususani kutokana na fedha za korosho ambazo kila mwananchi atalazimika kuchangia.
Sambamba na hilo Mtatiro amewataka wananchi kufahamu kuwa TImu hiyo ni wananchi wote wa Tunduru,hivyo wanapaswa kuiunga mkono kwa kuchangia fedha ili iweze kujiendesha na kufanya vizuri katika mashindano yajayo ya LIgi daraja la pili Taifa.
Katika hatua nyingine mkuu wa wilaya amesema, kwa kushirikiana na Chama cha Mapinduzi watahakikisha wanaufanyia ukarabati mkubwa Uwanja wa michezo wa CCM wilaya unaotumika kwa ajili ya michezo mbalimbali ya mpira wa miguu ili uwe bora na utumike kwa ajili ya ligi inayokuja.
Alisema, ukarabati wa uwanja huo utafanyika kabla ya kuanza kwa Ligi Daraja la pili ambapo Timu ya Tunduru Korosho itashiriki baada ya kuibuka mabingwa wa ,Ligi ya Mabingwa Taifa mashindano yaliyozishirikisha Timu 8 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.
Kwa upande wake,mwenyekiti wa Timu ya Tunduru Korosho Mohamed Kiyonjo amewashukuru wakazi wa mji wa Tunduru kwa kujitokeza kwa wingi kuipokea timu hiyo na kusema kuwa hali hiyo imeleta hamasa kwa wachezaji wa timu hiyo kufanya vizuri zaidi katika mashindano yajayo.
Kiyonjo alisema, ni faraja kubwa kuona idadi kubwa ya wananchi wamejitokeza kuipongeza na kuipokea timu yao ambapo ametumia nafasi hiyo kuwaomba wana Tunduru kuendelea kuiunga mkono Timu ili iweze kufanya vizuri zaidi katika michezo yake.
Hata hivyo,amekiomba Chama cha Mapinduzi kuharakakisha kuufanyia ukarabati uwanja wa michezo wa CCM ambao utatumika kama uwanja wa nyumbani kwa Timu hiyo.