Kaimu Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili Tanzania Consolata Mushi akitoa taarifa kwa Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe kuwa taasisi yake tayari imekwisha sajili jumla ya wahitimu 1224 katika kanzidata ya wataalamu wa mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa wageni,leo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa wahadhiri wa Kiswahili katika chuo kikuu cha Dodoma.
……………………………………………………………………………………….
Na. Anitha Jonas – WHUSM, DODOMA
Baadhi ya watanzania wamekuwa na hulka ya kutokuwa na matumizi sahihi ya baadhi ya maneno ya lugha ya Kiswahili, hali ambayo imesababisha Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) ikiwa ni taasisi yenye dhamana kuanza kutoa elimu sahihi yamatumizi ya maneno ya lugha hiyo.
Kaimu Katibu Mtendaji wa BAKITA Bibi. Consolata Mushi, hivi karibuni alipokuwa akizungumza kwa njia ya simu na Afisa Habari wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Habari, Bibi. Anitha Jonas alisema kuwa baadhi ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili wamekuwa wakifanya makosa ya matumizi ya lugha ya Kiswahili.
Aidha, Bi.Consolata alisema kuwa baadhi ya maneno yamekuwa yakitumiwa kimakosa na utumiaji huo umepelekea kuibua mgogoro wa kifikra miongoni mwa watumiaji wa lugha husika hivyo kuepukana na madhara yanayoweza kuwa makubwa ni bora kusahihisha matumizi hayo.
“Nitoe mfano ambao ulisikika siku moja kupitia chombo fulani cha habari kuwa mtaalamu wa kilimo amewaasa wakulima kutumia mbolea, utumiaji wa namna hii si tu kwamba unapotosha bali unaharibu kabisa dhana nzima ya kile kinachosemwa,”alisema Bibi.Consolata
Akitolea mfano wa maneno ambayo yanapotoshwa ni neno ‘asa’ kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili (2015) lina maana ya “Kanya au kataza mtu kufanya jambo fulani”, na kusema kuwa matumizi hayo yanaweza kupotosha na kuharibu maana ujumbe uliokusudiwa.
Vilevile, Bibi.Consolata alifafanua matumizi sahihi ya neno ‘asa’ kuwa linaweza kutumika kwa kuonya mfano: “Walimu wamewaasa wanafunzi kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya” au “Serikali yawaasa wazazi wanaowaachisha watoto wao shule kwa ajili ya kuwaoza.
Kwa mujibu wa BAKITA neno lingine ambalo limekuwa likipotoshwa na watumiaji wa lugha ya Kiswahili ni mrabaha, chanzo cha upotoshaji wa neno hilo ni ubadilishaji wa mpangilio wa vitamkwa vya mwisho vinavyounda neno hilo, badala ya kusema mrabaha watu husema mrahaba.
Mrabaha maana yake ni, “Malipo yanayotolewa na mchapishaji kwa mtunzi wa kitabu kwa kipindi fulani kama sehemu ya mauzo ya kitabu kinachohusika, au inaweza kuwa ni “Malipo yanayotolewa kama sehemu ya faida inayotokana na biashara fulani.
Halikadhalika, neno mrahaba halina maana yoyote katika lugha ya Kiswahili hivyo utumiaji wa neno hilo ni upotoshaji na watu wengi wamekuwa wakifanya makosa katika matumizi yake.
****************MWISHO****************