………………………………………………………………………………
Na Shamimu Nyaki.
Upashanaji habari katika Dunia ya sasa umebadilika. Teknolojia ya habari na mawasiliano imewezesha taarifa kumfikia mtu kiganjani kupitia simu muda ule ule tukio linapotokea ikiwa imeabatana na picha mnato au video.
Kutokana na hilo vyombo vya habari vya zamani kama redio na televisheni navyo vimebadilika kutoka mfumo wa kurusha habari zilizopitwa na wakati hasa matukio ambayo yalikwisharushwa na mitandao ya kijamii jana yake.
Mabadiliko haya yalililazimu Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kubuni mfumo mpya wa uhabarishaji ambao ulipewa jina la ARIDHIO (ikiwa na maana: habarisha, toa taarifa).
Siku za nyuma Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, alizindua rasmi ARIDHIO ambayo ni ndoto yake ya siku nyingi kufuatia kauli yake aliyowahi kuitoa Bungeni jijini Dodoma kwamba siku moja TBC itakuwa zaidi ya vyombo vikubwa vya kimataifa ikiwemo CNN na BBC.
ARIDHIO ni sehemu pekee ambayo mwananchi anaweza kupata habari zenye uchambuzi wa kina kutoka kwa wachambuzi wenye weledi na uzoefu mkubwa katika masuala mbalimbali ikiwemo siasa, uchumi, teknolojia, afya, michezo na burudani.
Katika ARIDHIO vipengele mbalimbali vinavyogusa nyanja zilizopo katika jamii vimepewa nafasi ikiwemo kipengele cha habari za biashara na kukiita SOKONI ili kutoa fursa kwa mwananchi wa kawaida kupata taarifa za bei za vyakula na mahitaji mengine muhimu kwenye masoko, kipengele cha michezo kimeongezewa muda zaidi na kuwa dakika 15 ambacho sasa kinaitwa JARAMBA.
Vipengele vingine ni HADUBINI ambayo ni habari za kina na siku ya Jumapili inatawaliwa na burudani zaidi ambapo saa moja kamili jioni inaanza JARAMBA SEREBUKA na kufuatiwa na KIOO ambacho kinakuletea ripoti mbalimbali na mjadala mrefu kuhusu maswala ya kijamii, urembo na utanashati, staili za maisha, mahusiano na kadhalika.
Mabadiliko haya yameifanya TBC kupitia ARIDHIO kuwa kituo kinachovutia na kuongeza idadi ya watazamaji na kuvivutia vyombo vingine vya habari kuweka mikakati ya kubadili mifumo yake ya utangazaji.
Mwisho