Home Michezo SIMBA SC YATWAA TAJI LA FA CUP (ASFC) MSIMU WA 2019-2020.

SIMBA SC YATWAA TAJI LA FA CUP (ASFC) MSIMU WA 2019-2020.

0

*Yavuna Pesa Taslimu za Kitanzania,   Milioni 50
*Mshambuliaji wa Panama,  Omar Yassin,  Mfungaji Bora wa Michuano.
*Chama Mchezaji Bora wa Michuano

……………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu,  Rukwa 
 
MABINGWA wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara,  Simba SC hatimaye wametwaa taji la Michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports Federation Cup (ASFC) msimu wa 2019-2020 baada ya ushimdi wa bao 2-1 dhidi ya Namungo FC katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Katika mchezo huo uliokuwa wa vuta ni kuvute dakika zote 90,  Simba SC ilianza mchezo kwa kasi nakufanikiwa kupata mabao hayo dakika ya 28 kupitia kwa Mshambuliaji wake, Luis Jose Miquissone wakati bao la pili likifungwa na Nahodha John Raphael Bocco dakika ya 39,  bao la Namungo likifungwa na Beki wa pembeni,  Edward Charles Manyama dakika ya 56.

Baada ya mchezo huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba Senzo Mbatha amesema Uongozi wa Klabu umefurahishwa na taji hilo sambamba na kuwapongeza Wachezaji wote na Benchi zima la Ufundi linaloongozwa na Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck  aliyefanikisha mafanikio hayo kwa timu.

Senzo amesema mipango ua usajili kwa timu hiyo unaendelea klabuni hapo,  amesema baada ya kumalizika kwa Michuano hiyo ya ASFC watakaa na Uongozi kujadili usajili na kuongeza Wachezaji wengine katika timu hiyo.

Naye Mfungaji wa bao la kwanza la mchezo huo wa Fainali,  Luis Miquissome amesema anafurahishwa na ushindi huo wa ASFC sambamba na Ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu licha ya kusajiliwa klabuni hapo katikati ya msimu.

Katika Michuano hiyo ya ASFC,  Kiungo Mshambuliaji wa Simba SC,  Cloutous Chama ‘Mwamba wa Lusaka’ ametwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Michuano hiyo.

Simba SC msimu huu wa 2019-2020 imejikusanyia mataji matatu ya Ngao ya Hisani,  Ligi Kuu Soka Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho (ASFC).