**********************************
NJOMBE
Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi UVCCM Mkoa wa Njombe hapo Jana Julai 30/2020 ilifanya Uchaguzi wa kumpata Mbunge wa Viti Maalumu atakaewakilisha Jumuiya hiyo Viti sita Upande wa Tanzania Bara.
Akizungumza mara baada ya mchakato wa uchaguzi kukamilika Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Njombe Ndg, Nehemia Tweve alisema Jumla ya Vijana watano wa kike walijitokeza kuomba nafasi hiyo ambao baada ya mchakato kukamilika Mmoja kati yao aliongoza kwa kupata kura nyingi akiwazidi wenzake Watano.
Tweve aliwataja Wagombea waliojitokeza kuomba nafasi hiyo kuwa ni Pamoja na Bi, Catherine Lusungu, Monica Norbert, Rehema Mahenge, Dorcas Kinyangadzi, na Bi, Deograsia Mbilinyi ambao walishiriki kikamilifu mchakato huo tangu hatua ya kwanza walipochukua na kurejesha Fomu.
Alisema jumla ya Wajumbe 21 walipigakura kati ya hizo Bi, Monica Norbert aliibuka Mshindi kwa kupata jumla ya kura 17 akifuatiwa na Bi, Catherine Lusungu aliyepata kura 03, Rehema Mahenge alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 02, Dorcas Kinyangadzi alipata kura 01 wakati Bi, Deograsia Mbilinyi akishika nafasi ya tano kwa kupata kura 0.
“Natoa wito kwa Vijana wote wa Njombe waendelee kutulia watambue kuwa tulichokifanya leo ni mapendekezo tu hakuna aliyeshinda hapa baada ya Chama ngazi za juu kumpitisha Mgombea mmoja kutoka Mkoa wa Njombe tutapaswa kumuunga Mkono haijalishi ameshika nafasi ya ngapi kwenye uchaguzi huu wa Maoni” Nehemia Tweve.
Bw, Thobias Omega Mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana Taifa anaewakilisha Mkoa wa Njombe alisema kura hizo ni maoni ya awali hivyo hakuna mshindi au aliyeshindwa hivyo Wagombea wote wanapaswa kuwa watulivu ikiwa pamoja na kuvunja Makundi ili kukipa Ushindi Chama Cha Mapinduzi kwenye nafasi hiyo Muhimu.
“Tulichokifanya leo ni kupiga kura za maoni haina maana kwamba amepatikana Mshindi wa Jumla hapana tunasubiri maamuzi ya Vikao vya Juu vitakavyopitisha Jina la Mgombea ambae ataenda kuwakilisha Mkoa wa Njombe kwenye Ubunge wa Viti Maalumu kundi la Vijana upande wa Tanzania Bara ambao tunazo nafasi sita” Thobias Omega.
Wakizungumza nje ya Ukumbi wa Ofisi ya CCM Mkoa wa Njombe Mshindi wa kwanza Bi, Monica Norbert na wa Pili Bi, Catherine Lusungu walisema wameridhishwa na mwenendo wa Mchakato huo mwanzo hadi mwisho hivyo wapo tayari kupokea uamuzi wowote wa Chama endapo utajitokeza baada ya Uchaguzi huo kukamilika.
“Naomba niwakumbushe Vijana wenzangu wa Njombe na Taifa kwa ujumla kuwa kushinda kura za Maoni sio kuwa Mbunge hapana naamini Chama bado kitaendelea na Vikao vya upembuzi zaidi, endapo mimi au mwingine atapitishwa sina tatizo zaidi nitaunga mkono uamuzi huo wa Chama” Monica Norbert aliyeongoza kura za Maoni Ubunge UVCCM Mkoa wa Njombe.
Bi, Amina Imbo Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe alisema kinachofuata baada ya Uchaguzi huo ni vikao vya mapendekezo ili kumpata Mgombea sahihi atakaekiwakilisha Chama ngazi ya Mkoa kwenye nafasi ya Ubunge wa Viti Maalumu kupitia Kundi la Vijana Viti sita upande wa Tanzania Bara.