Msajili wa Bodi ya Usajili Wataalamu wa Mipango Miji Hellen Mtutwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya siku mbili ya Wataalam wa Mipango Miji nchini tarehe 29 Julai 2020 jijini Dodoma. Wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ezekiel Mpanda ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi mafunzo hayo.Baadhi ya Washiriki wa mafunzo ya Siku mbili ya Wataalamu wa Mipango Miji nchini wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo tarehe 29 Julai 2020 jijini Dodoma.Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ezekiel Mpanda akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya siku mbili ya Wtaalam wa Mipango Miji kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Makao makuu iliyofanyika jijini Dodoma tarehe 29 Julai 2020 jijini Dodoma (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)
*******************************
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Serikali imewataka wataalamu wa Mipango Miji nchini kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia taaluma ili kuepukana na malalamiko yanayoendelea kutolewa na jamii kuhusiana na masuala ya mipango miji.
Kauli hiyo imetolewa tarehe 29 Julai 2020 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ezekiel Mpanda kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo Mary Makondo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa wataalam wa Mipango Miji nchini.
Alisema, udhaifu wa baadhi ya Wataalamu wa Mipango Miji nchini katika kusimamia utekelezaji wa sheria zilizopo kuhusiana na masuala ya mipango miji umesababisha baadhi ya miji kutopangika vizuri kama ilivyo kwenye nchi nyingine duniani na hivyo kuzua malalamiko kutoka kwa wananchi.
’’Napenda kutumia nafasi hii kuwaasa watumishi wenzangu kufanya kazi kwa uadilifu na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utendaji kazi zilizopo’’ alisema Mpanda.
Akigeukia upande wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Miapngo Miji, Mkurugenzi huyo wa Sera na Mipango aliitaka bodi hiyo kutekeleze majukumu yake ya usimamizi wa taaluma ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua stahiki wote wanaokiuka sheria, kanuni na maadili ya taaluma.
Kwa mujibu wa Mpanda, kwa muda mrefu sasa imeshuhudiwa malalamiko katika maeneo mbalimbali nchini kuhusiana na kazi za kimipangomiji hususan urasimishaji unaoendelea kufanyika nchini na kusisitiza kuwa Wataalam wa mipangomiji mmeacha jukumu la msingi la kufanya upangaji na badala yake mmeachia makampuni binafsi pekee kufanya kazi hizo na mbaya zaidi bila usimamizi madhubuti na kufanya makampuni hayo kupokea fedha nyingi kutoka kwa wananchi kwa ajili ya kufanya kazi walizoingia mikataba na Mamlaka za Upangaji lakini hayajakamilisha kazi zao.
Ameshangazwa na Wataalam wa Mipango Miji kuwaacha wananchi wakivunja sheria za ujenzi mijini na kueleza kuwa baadhi yao wanafanya hivyo kwa kutojua sheria na taratibu na kusema kuwa wananchi hao wanahitaji kuelekezwa kwa kuwa hawafanyi hivyo makusudi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius Kalimenze alisema, mafunzo hayo ya siku mbili ya wataalamu wa Mipango Miji kutoka katika mikoa na makao makuu ya Wizara yatasaidia kujua changamoto na miongozo ya uaandaji mipango iliyopitwa na wakati na kuongeza kuwa kwa sasa hapa nchini kumekuwa na changamoto mbalimbali kama vile mafuriko na kusisitiza kuwa wataalamu wa mipango miji wanatakiwa kujua namna ya kushiriki kuzitatua changamoto hizo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili Watraalamu wa Mipango Miji Profesa Wibroad Kombe alisema bodi yake ina wajibu wa kujenga uwezo kwa wataalamu wa mipango miji ili kuweza kukabiliana na changamoto za upangaji miji nchini ikiwemo katika maeneo ya uwekezaji wa ardhi ambapo mipango miji imekuwa sehemu ya tatizo.