Umoja wa Ulaya (EU) kupitia mradi wa upembuzi yakinifu wa miundombinu ya kusafirisha na kupoza umeme umeandaa mafunzo ya siku nne kwa wataalam 25 kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Lengo la mafunzo ni kuwajengea uwezo na ujuzi wa kusanifu na kusimamia ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme wa msongo mkubwa na vituo vya usambazaji na upozaji wa umeme.
Akizungumza siku ya ufuguzi wa mafunzo hayo siku ya tarehe 27 Julai 2020 ambayo yanafanyika katika hoteli ya Habour view jijini Dar es Salaam kwa njia ya video, Mkufunzi Mkuu Ndugu Stefano Galantino wa Kampuni ya Studio Pitrangeli ya Italia alisema kuwa mafunzo haya yanatoa fursa kwa wataalam hao kuongeza uwezo na ujuzi katika kusanifu miradi ya njia za umeme wa msongo mkubwa.
Mafunzo hayo yanaendeshwa na Kampuni ya Studio Pietrangeli ambayo ni Mshauri Muelekezi ambaye amepewa kazi ya upembuzi yakinifu na Serikali ya Tanzania kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).
Upembezuzi huu ni wa kimkakati ili kuwezesha kupanga na kutekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini kwa kuongeza wigo wa mtandao wa gridi ya Taifa. Wigo wa mradi huu utahusisha kusanifu na michoro ya takribani kilomita 2550 za njia za msongo mkubwa wa umeme, vituo 51 vya kupoza na usambazaji umeme vijijini ambapo vituo 36 ni vipya na vituo 15 vitaongezewa uwezo wa kupoza na kusambaza.
Awali mafunzo haya yalipangwa kufanyika mjini Rome nchini Italia zilipo ofisi za Mshauri Muelekezi hata hivyo kutokana janga la ugonjwa wa Korona yamefanyika nchini kwa njia ya video. Mada zinazotolewa ni miundombinu ya kusafirisha umeme umeme wa msongo mkubwa, tathimini ya vituo vya kupoza na kusambaza umeme, kusanifu miundombinu hiyo pamoja na tathimini ya uchumi na fedha katika mradi huo.
“Mafunzo haya yatatupa fursa ya kuongeza ujuzi katika kutathimini na kusanifu miundombinu ya kusafirisha na kupoza umeme” alisema MhandisiJensen Mahavile kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Kwa zaidi ya muongo mmoja Umoja wa Ulaya umekuwa ukishirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha na kuongeza upatikanaji huduma ya umeme kwa kufadhili miradi mbalimbali ya umeme, matumizi bora ya nishati, nishati jadidifu na nishati bora ya kupikia.