……………………………………
Na John Walter,BABATI
MKUU wa mkoa wa Manyara Joseph Mkirikiti amesema Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa, ambaye ametangulia mbele ya haki, kipindi cha utawala wake aliimarisha sana uchumi na utawala.
Mkirikiti alieleza hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya namna alivyomfahamu mzee Mkapa.
“Nchi yetu iliimarika sana kiuchumi, kiutawala na kimichezo kwa kuwa alitujengea uwanja wa Taifa,”Alisema Mkirikiti
Aidha alisema katika kipindi cha uongozi wake ulikuwepo ukomavu wa kisiasa ambao aliuimarisha.
Vile vile alisema atamkumbuka kwa kuwa Mkirikiti miaka ya 1991 akiwa chuo kikuu cha Dar Salaam na Rais wa chuo wakati huo Mkapa akiwa waziri wa sayansi na teknolojia alienda kuongea naye kuhusu masuala ya mikopo ya elimu ya juu na alimsikiliza vizuri pamoja na wenzake.
Alifafanua kuwa maisha yake yalikuwa sadaka kwa watanzania na mbali na sadaka aliuishi uongozi wake na alidai maisha yake yalikuwa mfano wa uongozi wake.
Hata hivyo alisema kipindi chake ndio vyombo vya habari viliongezeka sana na alikuwa anatoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari kila mwezi.
Mkazi wa Bagara Abdi Mdinku alisema atamkumbuka Mkapa kwa kuugawa mkoa wa Arusha na wakapata mkoa wa Manyara ambapo kwa sasa wanapata maendeleo kutokana na fursa zinazojitokeza.
Mdinku alisema kitu kingine anachokikumbuka ni kuwajengea watanzania uwanja wa Taifa ambao ni wa kisasa.