Aliyekuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa mwaka 2007/2012 wa Mkoa wa Manyara, Cosmas Bura Masauda akijieleza kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM Wilaya ya Babati Mji ili kuomba kuchaguliwa katika kura za maoni kugombea ubunge wa jimbo la Babati Mjini.
…………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Babati
Aliyekuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa kupitia Mkoa wa Manyara mwaka 2007/2012 Cosmas Bura Masauda ambaye aligombea kura za maoni ya ubunge wa jimbo la Babati Mjini kisha wajumbe wakampa kura moja amesema yupo tayari kupeperusha bendera ya CCM pindi jina lake likirudishwa na CCM.
Masauda akizungumza Julai 27 amesema yupo tayari kupeperusha bendera ya chama hicho kupitia jimbo la Babati Mjini kwani hatawapa kazi kubwa viongozi kumuuza kwa wananchi tofauti na wengine.
Masauda ambaye alisimamishwa uanachama mwaka 2016 na kurudishiwa kadi ya CCM Julai 14 mwaka huu kisha uchaguzi wa kura za maoni ukafanyika Julai 22 alipata kura moja ya wajumbe.
“Mimi baadhi ya viongozi walinisimamisha wakidai kuwa sikumuunga mkono mgombea ubunge wa CCM wa mwaka 2015 Kisyeri Werema Chambiri na madiwani wa kata tano jambo ambalo siyo la kweli kwani nilikuwa napinga udhalimu, rushwa na viongozi kuwa na wagombea wao mfukoni mwao,” amesema Masauda.
Amesema alirudishwa CCM siku ya kuchukua fomu Julai 14 na kwenye uchaguzi Julai 22 akapata kura moja, amewashukuru wajumbe kwani hakufanya kampeni ila wenzake walianza miaka miwili iliyopita na kuambulia kura tatu, mbili hadi sifuri.
“Mambo yaliyofanyika kwa wajumbe kwenye kura ya maoni yanatisha kwani kama huna pesa usijaribu ubunge ila namwomba Mungu jina lirudi ambalo litakuwa sahihi kwa wananchi atupe mbunge atakae kubalika na jamii nzima ya Babati mjini,” amesema Masauda.
Amesema wajumbe siyo kipimo cha kumpata mgombea mbunge kwani wasiokuwa na fedha waliambuliwa kushangiliwa kwa maelezo na kuambiwa muda, muda, na ana amini vikao vya juu vitaamua kwa umakini mkubwa mno.
Amesema viongozi wa CCM wa mkoa wanapaswa kutumia weledi wao katika kung’amua madhambi yaliyofanyika na kutoa haki kabla ya kwenda ngazi za CCM Taifa.
“Kuna watu wanasema hadharani kuwa wameshamaliza kamati kuu ila watambue kuwa wananchi wana macho na watu wa Babati wana misimamo yao naomba yasije ya mwaka 2015 yakajirudi, tulipoteza jimbo na madiwani watano nampongeza Rais Magufuli kwani akigundua jambo hana rafiki ni refa mwenye kadi nyekundu tuu njano hana nawasikia wananchi wanasema walionunua wajumbe wakimleta kwao itakula kwao ila wakimleta aliyepita buree na wao tutampa bure CCM hoyee,” amesema.
Amewaomba wanaotafuta kura hivi sasa ili majina yao yarudishwe waache mpaka Rais mstaafu wa awamu ya nne Benjamin Mkapa atakapozikwa kwani aliyefariki ni mtu muungwana aliyekataa malofa kuchukua nchi na msiba huo ni mkubwa kwani watanzania wapo kwenye ibada katika msiba huu mkubwa.
Amesema yupo tayari kupitishwa na kusimamishwa kugombea ubunge wa jimbo la Babati Mjini kwani hatawapa kazi kubwa ya kunadiwa na pia vijana watampitisha kwa miluzi.
Amesema anajulikana kwa misimamo isiyoyumba katika kupinga rushwa, hana unafiki, amenyooka na fitina kwake ni mwaka.
“Mchakato wa uchaguzi ulitawaliwa na rushwa yaani vyuma viligongana siyo benki siyo simu ni kurushiana muamala tuu kwa baadhi ya wagombea na wajumbe na usiposema sasa kipindi cha Rais Magufuli tutasema lini tena, tusipozungumza hivi sasa tunaongea kwenye utawala upi?” amehoji Masauda.