Askofu Mkuu wa Kanisa la TAG, Dkt. Barnabas Mtokambali (wa pili kushoto) akikata utepe ikiwa ni ishara ya kufungua rasmi kanisa la TAG CANA lililopo Ilazo, jijini Dodoma, jana. (Picha na Mpiga Picha Wetu)
Waumini wa kanisa la TAG CANA lililopo Ilazo, jijini Dodoma wakiomba kabla ya hafla ya kuwekwa wakfu kwa kanisa hilo jana. Hafla hiyo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la TAG, Dkt. Barnabas Mtokambali. (Picha na Mpiga Picha Wetu)Askofu Mkuu wa Kanisa la TAG, Dkt. Barnabas Mtokambali (kushoto) akizungumza baada kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa kituo cha watoto pamoja na kuweka wakfu kanisa la TAG CANA lililopo Ilazo, jijini Dodoma, jana. Kulia ni Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo, Dkt. Joel Hamuli pamoja na Mkewe Mchungaji Faraja Hamuli. (Picha na Mpiga Picha Wetu)
*********************************
*Asisitiza Watanzania walinde tunu ya amani na utulivu
*Aonya wasikubali kutumika kama vichaka vya maadui
*Asema Makao Makuu ya TAG yatahamia Dodoma
ASKOFU MKUU wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Dkt. Barnabas Mtokambali amewataka waumini wa kanisa hilo na Watanzania wote wajitoe kuombea uchaguzi mkuu ujao.
Ametoa wito huo leo (Jumamosi, Julai 25, 2020) wakati akizungumza na washiriki waliohudhuria ibada maalum ya kuweka wakfu kanisa la TAG CANA lililopo Ilazo, jijini Dodoma. Pia aliweka jiwe la msingi la kituo cha watoto cha kanisa hilo.
“Mwaka huu tuna uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais. Kama kanisa tunao wajibu kwa Taifa letu, nao ni maombi. Niwaombe wana-TAG na Watanzania wote kila mmoja aombe uchaguzi ili tuweze kuvuka kwa amani kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.”
“Kila nchi ina maadui wake na hasa nchi yenye utajiri mwingi kama yetu, wao hutumia muda kama huu wa uchaguzi ili kupenyeza mabaya yao. Kwa hiyo, uchaguzi unaweza kulijenga Taifa au kulibomoa, na sisi tukiomba Taifa letu haliwezi kubomoka,” amesema.
Amesema kila mmoja anao wajibu wa kuiombea Tume ya Uchaguzi ili iweze kuzingatia haki; kuombea vyama vya siasa kwani maadui wengi hujipenyeza kupitia huko. “Ombea kisiwepo chama cha siasa ambacho kitatumika kama kichaka cha maadui kwa sababu wagombea wote wanatoka huko,” amesisitiza.
Amewataka pia Watanzania wote wamuombe Mungu ili viongozi wanaochaguliwa wawe ni chaguo la Bwana. “Tumuombe Mungu ili tupate viongozi bora, siyo bora viongozi tena wanaotoka kwa Bwana,” ameongeza.
Ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania wadumishe amani na utulivu kwani ndiyo tunu za Taifa. “Amani na utulivu ndiyo tunu yetu. Wana-TAG na Watanzania wote tusikubali kutumika kuvuruga amani, tusikubali kushiriki jambo lolote litakaloondoa amani ili tuvuke tukiwa na umoja na mshikamano,” amesisitiza.
Wakati huohuo, Dkt. Mtokambali amewataka waumini wa kanisa hilo waendelee kuombea Mkutano Mkuu wa Wachungaji wote wa TAG unaotarajiwa kufanyika Agosti 12-14, mwaka huu jijini Dodoma. Wajumbe wa mkutano huo pia watapata fursa ya kumchagua Askofu Mkuu atakayeongoza kanisa hilo kwa miaka mingine minne.
“Tuendelee kuomba ili tuwe na mkutano wenye baraka na mafanikio. Tukumbuke kuwa viongozi wa Kanisa hawatokani na kampeni za kibinadamu bali wanatoka magotini. Tukiomba, Mungu anaweka mzigo kwa wachungaji na kuwaonesha nani anafaa kuwa Askofu Mkuu, Makamu wa Askofu, Katibu Mkuu au Mweka Hazina. Kama yuko mtu anazunguka na kusema Mtokambali anamtaka fulani awe Askofu hao ni waongo, na ni wazushi na mimi sijawatuma,” amesisitiza.
“Namtaka Mungu na nguvu zake zitupe Askofu Mkuu wa moyo wake, Makamu Askofu wa moyo wake… na mapenzi yangu mimi yavunjike na ya kwako yavunjike bali ya Mungu yasimame. Ninawaomba sana WaTAG wenzangu tusikubali kuingia kwenye kampeni za kibinadamu; sisi ni kanisa la kiroho na viongozi wetu wanatoka kwa Baba mbinguni.”
Katika hatua nyingine, Askofu Mkuu Dkt. Mtokambali amesema kanisa la TAG linapanga kuhamia Dodoma sababu ya kukua kwa gharama za uendeshaji kutokea Dar es Salaam. “Japo makao makuu ya TAG yako Dar es Salaam, kazi nyingi zinafanyika hapa Dodoma, inatugharimu sana kuja na kurudi kuonana na viongozi wa Serikali. Tumefanya maamuzi ya haraka ili ifikapo Septemba mwakani, tuwe tayari tuko Dodoma.”
Mapema, Naibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Bw. Anthony Mavunde amesema anafarijika kuona kanisa linasaidia juhudi za Serikali za kuweka miundombinu ikiwemo maeneo ya kuabudia.
“Tunaijenga Dodoma siyo kwenye miundombinu ya barabara tu, bali hata sehemu za kuabudia. Mtu akija Dodoma aone tofauti, hawezi kuona makao makuu ya nchi halafu nyumba zake za ibada zinakuwa za kawaida. Nawapongeza kwa jengo hili zuri la kanisa ambalo mmetumia michango yenu na sadaka zenu badala ya kutegemea wafadhili kutoka nje,” amesema.
Naibu Waziri Mavunde ambaye alialikwa kwenye ibada hiyo, amewataka waumini wamuombee Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuipa heshima kubwa Dodoma kwani kila kitu kizuri na cha mfano hapa nchini hivi sasa kinapatikana Dodoma.
“Ukiondoa Afrika Kusini, Dodoma imepata barabara ya mzunguko ya kilometa 112.3 yenye njia nne ambayo ikikamilika itaondoa msongamano katikati ya jiji. Tumepata soko kubwa la kisasa la Job Ndugai; tuna stendi ya kisasa yenye uwezo wa kuingiza magari 600. Tunasubiri uwanja wa mpira wa kisasa, uwanja wa ndege wa Msalato ambao barabara yake itakuwa na urefu wa kilometa tatu, ndefu kuliko viwanja vyote nchini,” amesema.
Mapema akisoma risala kuhusu ujenzi wa kanisa na kituo cha watoto, Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo, Dkt. Joel Hamuli alisema ujenzi wa kanisa hilo ambao ulianza Aprili 16, 2018 na kukamilika Juni 2019, umegharimu sh. milioni 98.
Kuhusu ujenzi wa kituo cha watoto, Dkt. Hamuli alisema ujenzi wake umefikia hatua ya linta na hadi sasa wametumia sh. milioni 15. “Kadri michango itakavyoendelea kupatikana, tunatarajia kukamilisha ujenzi wake ifikapo Desemba, 2020,” alisema.