Mkuu wa dawati la elimu kwa umma TAKUKURU Mkoani Manyara, Sultan Ng’aladzi akitoa mada ya athari za rushwa.
…………………………………………………..
Na Mwandishi wetu, Babati
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Manyara imewataka wadau wanaotumia barabara za Mkoa wa huo, kutunza miundombinu ya barabara kwani Serikali itatumia gharama kubwa kufanya ukarabati.
Mkuu wa dawati la elimu kwa umma wa TAKUKURU mkoani Manyara, Sultan Ng’aladzi ameyasema hayo jana mjini Babati.
Ng’aladzi ameyasema hayo wakati akizungumza na wadau mbalimbali wa barabara wa mkoa huo.
Akitoa mada ya athari za rushwa kwa watumishi wa TANROADS kitengo cha mizani amesema watumishi wanapaswa kuwa waadilifu katika utendaji kazi wao.
Amewataka watumishi hao kujiepusha na vitendo vya kuharibu kamera na mizani ili kuwezesha wasafirishaji kupita kwenye mizani kwa kukwepa tozo za mizigo inayozidi.
“Kwa kuwa vitendo hivyo husababisha upotevu mkubwa wa mapato ya Serikali kwa rushwa kidogo wanayopokea na pia vitendo hivyo husababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara,” amesema.
Amesema vitendo hivyo husababisha hasara kutokana na kupitisha mizigo mizito kuliko ilivyokusudiwa kwenye barabara kwani matengenezo yake hugahrimu Taifa fedha nyingi.
Semina hiyo iliwahusisha wadau wa usafiri na usafirishaji wakiwemo wamiliki wa magari ya mizigo na abiria na askari wa usalama barabarani.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo waliopongeza TAKUKURU kwa namna wanavyotoa huduma ya elimu kwa wadau wa barabarani.