…………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma Godwin Mkanwa amesema kuwa chama hicho kitamuenzi Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Benjamin Wiliam Mkapa (1995-2005), kwa yale aliyoyafanya katika utawala wake hasa katika kujenga msingi wa uchumi wa nchi.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma baada ya kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya CCM, Benjamin Wiliam Mkapa (1995-2005), kilichotokea usiku wa kuamkia jana.
Aidha Mkanwa amesema kupitia itikadi ya Marehem Mkapa ya uwazi na ukweli, Mkapa aliweka mambo mengi kwa uwazi kwa kusimamia misingi na shabaha za uongozi uliotukuka kwa kusimamia mapato ya nchi .
“Kubinafisha mashirika ya umma kulichochea kuleta maendeleo kutokana na sekta binafsi kuendesha mashirika hayo na kuisaidia serikali kujiendesha kiuchumi ” amebainisha Mkanwa.
Kwa upande wa baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Dodoma wamepata nafasi ya kutoa maoni yao jinsi walivyopokea taarifa za msiba wa Mzee Mkapa ambapo wamesema kuwa ni pigo kwa watanzania na Nchi za Afrika.
Naomi Godwin ametoa yake ya moyoni kuwa alimfahamu Mkapa katika utawala wake alikuwa ni mtu aliyejishughulisha katika masuala ya usuluhishi wa migogoro kwa baadhi ya mataifa na kuacha alama ya amani kwa mataifa mengine ikiwemo Kenya na Burundi.
“Watanzania tutamkumbuka kwa kuenzi heshima na busara zake ,ametuachia tunu kubwa ambayo itaishi vizazi na vizazi pale alipozindua kitabu chake cha My Life My Purpose,”ameeleza Naomi.