**************************************
Na Masanja Mabula , Pemba
FAMILIA za wahanga wa udhalilishaji kisiwani Pemba wameshukuru na kupongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA_Zanzibar za kupambana na vitendo vya udhalilishaji katika jamii.
Pongezi hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti na baadhi ya wanafamilia hao mara baada ya kukabidhiwa Kuku na chama hicho kwaaajili ya uguaji ikiwa ni sehemu ya juhudi za chama hicho kupambana na vitendo vya udhalilishaji.
Mmoja wa wanufaika wa msaada huo Bi Mpemba Ali Moh’d amesema Kuku hao watawasaidia kujiendeleza kiuchumi kulingana na hali ngumu ya maisha wanayokabiliana nayo.
“Tunawashukuru sana watu wa TAMWA kwa kutambua matatizo yetu na kuamua kutuletea msaada huu wa Kuku kama sehemu ya faraja kwetu, tunajisikia furaha sana kwakweli leo,” alisema.
Aidha aliongeza kuwa kutokana na familia hizo kuwa katika hali ngumu ya maisha kupitia ufugaji wa Kuku itawawezesha kurahisisha upatikanaji wa huduma za msingi katika familia zao.
“Kupitia Kuku hawa tuliopewa leo watatusaidia sana kututalulia shida nyingi majumbani mwetu kama vile chakula kulingana na hali zetu ndio kama hivo hatujiwezi na hatuna shughuli nyingine yoyote ya kutupatia kipato,” alisema Mpemba.
Kwa upande wake Shaali Makame Sahaali amesema licha ya Kuku hao kuwasaidia kujiendeleza kiuchumi lakini pia imechochea hamasa kwa familia hizo kujiona kuwa sehemu ya jamii kulingana na hali zao.
“Niseme tu kwamba TAMWA imefanya jambo kubwa sana leo kwani licha ya mitihani tuliyokumbana nayo lakini kupitia hili nasisi tumefarijika sana na kujiona kuwa sehemu ya jamii,” alisema.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, katibu wa Sheha ya Kiwani Wilaya ya Mkoani, Mohamed Haji Suleiman alishukuru mchango wa TAMWA Zanzibar katika kulinda na kutetea haki za kijamii Zanzibar na kukitaka chama
hicho kuendelea na juhudi hizo ili kuhakikisha jamii inabaki salama.
“Juhudi hizi zinazoendelea kuchukuliwa na TAMWA si kazi ndogo. Niwaombe sana endeleeni na juhudi hizi ili kuhakikisha mnasaidia kutokomeza vitendo vyote vya udhalilishaji katika jamii zetu Zanzibar,” alisema.
Mapema mratibu wa TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said
amesema lengo la kutoa msaada wa Kuku kwa familia za wahanga wa vitendo
vya udhalilishaji ni kuwawezesha kuwa na shughuli za kujiingiza kipato
katika familia.
“Tumeamua kutoa msaada huu kwa familia hizi ili uwasaidie kuendesha
familia zao kutokana na wengi wao kuwa katika hali ngumu ya maisha,”
alisema.
Aidha mratibu huyo ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa
mradi wa kupinga udhalilishaji Zanzibar katika kuwawezesha wahanga
kujihusisha na shughuli za uzalishaji ili kuwa na uwezo wa kufuatilia
kesi zao mahakamani.
Alisema, “miongoni mwa malengo ya kutolewa kwa Kuku hawa ni kuwawezesha
kupata shughuli ambayo itawasaidia kupata kipato cha kufuatilia kesi
zenu ili muweze kupata haki zenu.”
Jumla ya Kuku 300 wamegawiwa kwa familia 30 za wahanga wa vitendo hivyo
kutoka Wilaya ya Mkoani na Wete Pemba.