*********************************
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
KATIKA Kura za maoni mkoani Pwani ,Upande wa UWT ,ubunge viti maalum ,Subira Mgalu ameshinda kwa kura 252 dhidi ya wagombea wenzake 26 waliojitokeza kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo .
Katika kinyang’anyiro hicho ,Hawa Mchafu na Zainab Vullu wamepata kura 227 ambapo wameshika nafasi ya pili .
Kinyang’anyiro hicho kilichoanzia asubuhi na kumalizika saa 9.30 alfajili ya Julai 24 ukumbi wa Filbert Bayi mjini Kibaha, chini ya usimamizi wa Aboubakary Kunenge Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, akisaidiwa na Lukhia Masenga Mwenyekiti wa (UWT) Wilaya ya Bagamoyo na Anastazia Amas Katibu wa CCM Mkoa wa Pwani.
Katika kinyang’anyiro hicho Mgalu alijinyakulia kura 252, Hawa Mchafu kura 227, Zaynab Vulu 227, Nancy Mutalemwa 102 huku Mwenyekiti wa UWT Mkoa Farida Mgomi akipata kura 58, huku wagombea wa nafasi zingine waliopigiwa kura katika nafasi zao walizoziomba.
Akitangaza matokeo Kunenge aliwataja washindi na nafasi zao ziko kwenye mabano kuwa ni Tabia Kalega (Wasomi 203), Zaynabu Gama (Taasisi Binafsi 312), Blandina Sengu (Walemavu 180), Dr. Halisi Kaijage (Wafanyakazi 160) .
“Nasisitiza kwamba washindi ambao tumewapata hapa ni hatua ya awali, majina yao yatapelekwa ngazi nyingine jijini Dodoma ambako huko kutakuwa na zoezi lingine linalofanana na hili “
Anastazia aliwataka viongozi wa chama hicho na Jumuiya kufuata utaratibu uliotumika kwenye uchaguzi huo katika uchaguzi wa Madiwani wa Kata na wa Viti Maalumu kwa lengo la kuepukana na malalamiko kutoka kwa washiriki.
Zoezi hilo lilikuwa na wagombea 43 katika nafasi za Ubunge wa Viti Maalumu uliogawanyika makundi matano ambayo ni la Wafanyakazi, Walemavu, Ngo’s, Wasomi na Viti Maalum nafasi tatu.