Beki tegemeowa timu hiyo Pascal Wawa alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 75 baada ya kuonyesha utovu wa nidhamu mbele ya refa Ludovic Charles wa Mwanza kwa kuudunda mpira chini kwa hasira kuashiria kukerwa na maamuzi ya refa kufuatia awali kuonyeshwa kadi ya njano kwa kucheza rafu dakika ya 69.
Hata hivyo, mabingwa mara 21 wa Ligi Kuu wakafanikiwa kumalizia mchezo wao wa 37 wa msimu bila kuruhusu bao, hivyo kufikisha pointi 85, sasa wakiwazidi pointi 16 watani wao wa jadi, Yanga SC wanaofuatia nafasi ya pili.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao pekee la Daruwesh Saliboko kwa penalty dakika ya 78 limeipa ushindi wa 1-0 Lipuli FC dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Samora mjini Iringa.
Uwanja wa Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Edward Songo akaifungia bao la kusawazisha JKT Tanzania dakika ya 50 ikitoa sare ya 1-1 na wenyeji, Polisi Tanzania waliotangulia kwa bao la Matheo Anthony dakika ya 32.
Alliance FC ikalazimishwa sare ya 2-2 na Ndanda SC kutoka Mtwara. Mabao ya Alliance yamefungwa na Israel Patrick dakika ya tisa na Martin Kiggi dakika ya 60, wakati ya Ndanda SC yamefungwa ya Abdul Khamis dakika ya 16 na Omary Mponda dakika ya 51.
Mchezo mwingine wa Ligi Kuu unaendelea hivi sasa kati ya wenyeji, Azam FC na Mbeya City Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Kikosi cha Coastal Union kilikuwa; Abubakar Ibrahim, Hassan Kibailo, Hance Masoud, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Ame, Salum Ally, Mtenje Albano, Ayoub Lyanga, Mudathir Abdallah/Shaaban Iddi dk83, Ayoub Semtawa na Issa Abushehe.
Simba SC; Beno Kakolanya, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Muzamil Yassin, Meddie Kagere, John Bocco/Clatous Chama dk69 na Miraj Athumani ‘Madenge’/Deo Kanda dk69.