****************************
Katibu Tawala Mkoa wa Songwe Dkt Seif Abdallah Shekalaghe amewasili rasmi leo katika ofisi za Mkoa wa Songwe na kupokelewa na viongozi mbalimbali pamoja na watumishi wa ofisi hiyo.
Mara baada ya Mapokezi hayo yalio ongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela, Dkt Shekalage amezungumza na watumishi wote wa Ofisi hiyo na kuwaahidi ushirikiano wa hali ya juu huku akiwa eleza kuwa katika utendaji wake hatoweza kumvumilia mtumishi yeyote ambaye si mwadilifu.
“Mtumishi asiye mwadilifu si rafiki yangu, lakini nawahakikishia katika utendaji wangu sitamuonea mtumishi yeyote isipokua akitenda maovu na nikipata ushahidi basi sheria itafuata mkondo wake”., amesema Dkt Shekalaghe.
Amesema anapenda watumishi wote wafanye kazi kwa ushirikiano, Umoja, uwazi uzalendo, uadilifu na kazi watakazofanya zilete matokeo chanya katika maendeleo ya Mkoa wa Songwe.
Dkt Shekalaghe ameongeza kuwa utendaji kazi wake utakuwa wa kufuata taratibu na sheria zote huku akiahidi kuwathamini watumishi wa ngazi zote kwani anaamini hata mtumishi wa ngazi ya chini anao mchango mkubwa katika maendeleo hivyo watumishi wawe huru kumuona wanapomuhitaji.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amemkaribisha Dkt Shekalaghe na kumuahidi ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake huku akiwataka watumishi wote kumpa ushirikiano wa kutosha bila fitna au matatizo yoyote.
Brig. Jen. Mwangela amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amemuamini Dkt Shekalaghe kuwa anao mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya haraka kwa Mkoa wa Songwe hivyo atumie uzoefu wake katika kuwasaidia wananchi wa Songwe.
MAELEZO YA PICHA
Katibu Tawala Mkoa wa Songwe Dkt Seif Abdallah Shekalaghe akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe (Hawapo pichani) mapema leo alipo wasili rasmi na kupokelewa na viongozi mbalimbali.
Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Songwe wakimsikiliza Katibu Tawala Mkoa wa Songwe Dkt Seif Abdallah Shekalaghe (Hayupo pichani) mapema leo alipokuwa akizungumza nao mara baada ya kuwasili leo.