………………………………………………..
Na Emmanuel J. Shilatu
Wana Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanafurahia namna ambavyo Serikali iliyopo madarakani inavyotekeleza ilani ya uchaguzi 2015 – 2020 ila wapo baadhi yao hawaridhishwi na mambo makuu mawili ambayo hayana afya kwa CCM.
Mosi; Wapo baadhi ya Wana CCM hawakuwa wanafurahishwa kitendo cha wanaotoka upinzani na kujiunga CCM hususani viongozi kupewa kipaumbele kwenye teuzi kubwa na fursa za kugombea, walikuwa wanalalamika mno kuwa wale walioitukana na kuwapa shida kwenye chaguzi wanaonekana wa maana zaidi kuliko wapiganaji ndani ya CCM. Sawa na Mtoto wa kambo kulazwa chumbani, huku wenye mji kulazwa stoo!
Ushahidi wa chukizo hili umejitokeza kwenye kura za maoni za kuomba ridhaa kugombea ubunge wengi wameangushwa vibaya. Si Nassari, si Kafulila, si Mtolea, si Lijuakali, si Silinde, si Katambi yaani wote wameangukia pua. Sawa unaweza kusema ndio demokrasia ila hapa Wana CCM wamecheua ya moyoni kupitia kura za maoni.
Pili; Wana baadhi ya Wana CCM wamekuwa na kilio cha kupewa nafasi ndogo ama kukosa kabisa kwa kutengwa kwenye nafasi kubwa za kiuteuzi ambazo ndizo zilikuwa halali yao (taratibu za miaka yote) na badala yake wakipewa Madokta na Maprofesa ambao hawana historia ya siasa, uongozi na mapenzi ya CCM. Hapa napo naona dalili mbaya za mkomoeni kwenye uchaguzi kupitia kususa na aina zote za hujuma kwa baadhi ya Wana CCM tena wakifanya kwa makusudi.
Kama waliweza kumshangilia Mtulia nje ila ndani ya sanduku la kura wakampa Tarimba hawatashindwa kufanya ndivyo sivyo kwenye uchaguzi huu Mkuu Oktoba 2020.
Ndugu yangu Mwana CCM Uchaguzi huu ni mwepesi sana kuliko chaguzi zote kwani Rais Magufuli ametekeleza kwa asilimia kubwa ilani ya uchaguzi kiasi cha Tanzania kuingia uchumi wa kati.
Ewe Mwana CCM chonde chonde vyeo ndani ya CCM haviishi vipo kila siku, teuzi zipo kila siku huu ndio wakati wa kushikamana kwa umoja wetu kuzisaka kura za kishindo za Madiwani wa CCM, Wabunge wa CCM na Marais wa CCM ili CCM iendelee kushika dola kwa kura za kishindo kikuu. Tuvunje makundi yetu na kuweka kando yote ya kutugawa na kutuvunja moyo.
Watu watapita ila CCM itakuwepo milele yote. CCM si mali ya Mtu ni taasisi yetu sote wenye mapenzi mema na CCM tunayo kila sababu ya kuipenda kwa dhati kwa kuitendea haki pasipo kujali fadhila na badala yake siku zote ujiulize umeifanyia nini CCM na sio CCM imekufanyia nini.
Shime Wana CCM kama tulivyoanza pamoja nayo, tuendelee pamoja nayo, tusiiseme CCM hadharani, tusiwachafue wagombea wetu mitaani au mitandaoni na badala yake tutumie taratibu za vikao kama jadi yetu kujadili mambo yetu.
Umoja wetu ndio nguzo na ushindi wetu CCM.
Kidumu Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Mungu ibariki Tanzania