Timu ya Yanga SC imerejea nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya Singida United usiku wa leo Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 67 na sasa inawazidi pointi mbili Azam FC baada ya wote kucheza mechi 35.
Simba SC, tayari mabingwa wakiwa na pointi zao 81 na kesho watacheza mechi yao ya 35 ya msimu dhidi ya Mbao FC ya Mwanza Uwanja wa Taifa.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na Martin Saanya aliyesaidiwa na Jesse Erasmo, wote wa Morogoro na Mohamed Mkono wa Tanga, mabao ya Yanga SC yamefungwa na beki Paul Godfrey ‘Boxer’ dakka ya 26, kiungo Mrisho Ngassa dakika ya 38 na mshambuliaji Muivory Coast, Yikpe Gislain dakika ya 69.
Bao pekee la Singida United iliyoinga kwenye mchezo wa leo ikiwa tayari imeshuka daraja limefungwa na Mghana, Stephen Sey dakika ya 45 na ushei.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Mtibwa Sugar imeichapa 1-0 Azam FC Uwanja wa nyumbani, CCM Gairo mkoani Morogoro, bao pekee la beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ dakika ya 38.
Namungo FC imeichapa Mbeya City 1-0, bao pekee la Abeid Athumani dakika ya 46 Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Pwani.
Na Uwanja wa Kaitaba, Bukoba bao la penalti la Awesu Awesu dakika ya 40 limeipa ushindi wa 1-0 Kagera Sugar dhidi ya Coastal Union ya Tanga.
Bao la Adam Adam dakika ya 90 na ushei likaipa sare ya 1-1 nyumbani JKT Tanzania dhidi ya Alliance FC ya Mwanza iliyotangulia kwa bao la David Richard dakika ya 36 Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Nayo Ndanda FC ikaichapa 2-1 Tanzania Prisons Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara. Mabao ya Ndanda yalifungwa na Vitalis Mayanga dakika ya 39 na Taro Donald dakika ya 51, wakati la Prisons limefungwa na Jumanne Elifadhili kwa penalti dakika ya 65.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Farouk Shikhalo, Paul Godfrey ‘Boxer’, Adeyoum Ahmed, Kelvin YOndan, Lamine Moro, Abdulaziz Makame, Mrisho Ngassa/Erick Kabamba dk75, Raphael Daudi/ Ditram Nchimbi dk37, David Molinga/ Yikpe Gislain dk61, Patrick Sibomana/Ally Mtoni dk61 na Deus Kaseke/ Adam Kiondo dk75.
Singida United; Owen Chaima, George Wawa, Edward Mshanga, Kazungu Mashauri, Erick Emmanuel, David Nartey, Seiri Arugumaho/ Ramadhan Hashimu dk86, Emmanuel Simon, Stephen Sey/Shaaban Hussein dk90+4, Stephen Opoku/Adolph Anthony dk86 na Emmanuel Manyama/ Angelo Mbilinyi dk90+4.