Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi, Anthony Sanga (mwenye Shati lenye Maya) akiangalia ramani ya mtandao wa mradi wa maji wa Ismani – Kilolo wakati alipotembelea kukagua miradi mbalimbali ya maji mkoa wa Iringa inayotekelezwa na serikali ya awamu ya tano.( Picha na Denis Mlowe).
*****************************************
NA DENIS MLOWE, IRINGA
ZAIDI ya wakazi 58,821 wa eneo la Mradi wa Maji Ismani -Kilolo wanatarajia kunufaika pindi mradi wa Tanki kubwa unaojengwa na Mamlaka ya majisafi na usafi wa Mazingira mkoa wa Iringa (Iruwasa) kwa kushirikiana na Wakala wa Majisafi na usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) pindi ukikamilika.
Mradi huo ambao unatumia fedha za ndani kiasi Cha sh. Bilioni 9.27 ukiwa na lengo la kuwaondolea changamoto ya maji wakazi wa vijiji 29 vitanufaika katika mradi huo ambapo vijiji 5 vya Kilolo na vijiji 24 vya Ismani vitapata maji Safi na Salama.
Akizungumzia mradi huo Meneja Ufundi,Injinia wa Iruwasa,Fabian Maganga mbele ya Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga alipofanya ziara ya kukagua miradi ya maji inayotekelezwa na serikali ya awamu ya tano chini jemedari John Magufuli.
Mhandisi Maganga alisema kuwa mradi huo unaotekelezwa na serikali kwa njia ya force akaunti utatatua changamoto ya ukosefu wa maji kwa wananchi wa vijiji hivyo ukiwa una uwezo wa kuzalisha lita milioni 4.1 kwa siku wakati uzalishaji ni 2.9 kwa siku kipindi Cha masika.
Alisema kuwa mahitaji ya maji yanatarajiwa kufikia wastani wa Lita milioni 4 .65 kwa siku ifikapo mwaka 2038 hivyo mradi huu utakuwa suluhisho kubwa kwa wakazi wa vijiji hivyo pindi ukikamilika.
“Mradi huu wa maji wa Isimani -Kilolo utahudumia wakazi wengi na tunaamiji itamaliza tatizo la maji kwa kuwafikia wananchi wengi zaidi watapata maji na kuondokana na kutembea mwendo mrefu kufuata maji”
Aliongeza kuwa mtandao wa maji una jumla ya km 157 na unatoa Huduma kwenye vitongoji 25 kwa Sasa ukiwa na matenki 25 yenye ujazo wa Lita 25,000 Hadi 150,000 ambapo hutolewa kupitia vituo 234 na muunganisho ya ndani 768.
Alisema kuwa mradi huo ambao umeanza rasmi April 15 unatarajiwa kukamilika Juni 30 2021 ambapo wizara ya maji imekwisha toa milioni 450 kwa ajili kuendeleza na ujenzi.
Kwa upande wake, Meneja wa Ruwasa mkoa wa Iringa mhandisi ,Shaban Jellan alisema kuwa mkoa wa Iringa unakabiliwa changamoto mbalimbali zikiwemo uhaba wa vitendea kazi Kama magari kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ambapo mahitaji ni magari 12 yaliyopo ni 5.
Alisema kuwa changamoto nyingine ni upungufu wa watumishi kwa ajili ya usimamizi na uendeshaji wa miradi ambapo mahitaji halisi ya mkoa ni wahandisi 18 waliopo ni 14 mafundi sanifu mahitaji ni 33 waliopo ni 11.
Naye Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Maji,Mhandisi, Anthony Sanga alitoa wiki 6 kwa Iruwasa na Ruwasa kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa njia mbadala wakati mradi wa maji Ismani – Kilolo unamalizika na kuanza kufanya kazi mara moja.
Aidha akitoa wiki nne kwa Mamlaka hizo kuhakikisha wananchi wa Pawaga wanapata maji Safi na Salama kutokana na mradi wa maji wa Pawaga kukamilika kwa asilimia 90 hivyo waache maji yatoke wakati mradi unakamilika ndani ya muda huo tofauti na muda wa miezi miwili waliotaka mhandisi wa Ruwasa.
” Mradi wa Maji wa Ismani – Kilolo Natoa wiki sita watu waanze kupata maji kwa njia mbadala wakati mradi huu unaendelea kujengwa kuliko kusubiri mradi ukamilike wakati wananchi wanapata tabu ya maji na natoa wiki nne kwa mradi wa maji wa Pawaga ukamilike na watu wapate maji “Alisema
Alisema kuwa mradi huo uanze kujengwa haraka iwezekanavyo huku wizara inatoa fedha nyingine kiasi Cha milioni 200 zitaingia Jumatatu ijayo na watu waanze kuchimba mitaro kwa ajili ya kuendelea na mradi.
Alisema kuwa vibarua watumike wazawa wa maeneo husika kwani inasaidia kuongeza ajira kwa wananchi ikiwa ni lengo la Rais Magufuli kuwaletea maendeleo na kuongeza ajira kwa vijana.