Na Mwandishi Wetu
MABINGWA wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba SC wamepoteza mchezo wa nne wa msimu baada ya kuchapwa 3-2 na Mbao FC usiku wa leo Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Hadi inatawazwa kuwa bingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya tatu mfululizo na 21 jumla, Simba SC walikuwa wamepoteza mechi tatu tu na zote wakifungwa 1-0 dhidi ya Mwadui 1-0 Shinyanga, Yanga SC na JKT Tanzania Dar es Salaam.
Pamoja na ushindi huo, Mbao FC inabaki nafasi ya 19 licha ya kufikisha ponti 38 baada ya kucheza mechi 35, wakati Simba SC wanabaki na pointi zao 81 za mechi 35 pia kileleni.
Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Nassor Mwinchui wa Pwani aliyesaidiwa na Charles Simon wa Dodoma na Hamdan Said wa Mtwara, hadi mapumziko Mbao FC walikuwa mbele kwa mabao 2-1.
Rajab Rashid aliifungia bao la kwanza Mbao FC dakika ya tano tu akimalizia mpira uliotemwa na kipa Ally Salum kufuatia shuti la Herbert Lukindo.
Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere akaisawazishia Simba SC kwa penalti dakika ya 34 baada ya Abdulrahman Said kumuangusha beki Gardiel Michael kwenye boksi.
Mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Waziri Junior akaifungia Mbao FC bao la pili dakika ya 45 akimalizia pasi ya Jordan John.
Kipindi cha pili Miraj Athumani ‘Masenge’ akaisawazishia tena Simba SC dakika ya 52 akimalizia pasi ya kiungo mwenzake mshambuliaji, Ibrahim Ajibu Migomba.
Mshambuliaji Jordan John akaifungia bao la tatu Mbao FC dakika ya 58 akimalizia kazi nzuri ya mfungaji wa bao la pili, Waziri Junior.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Ally Salum, Haruna Shamte/Deogratius Kanda dk65, Gardiel Michael, Yussuf Mlipili, Erasto Nyoni, Said Ndemla, Hassan Dilunga, Muzamil Yassin, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu na Miraji Athuman ‘Madenge’/ Shiza Kichuya dk77.
Mbao FC; Rahim Shekhe, Datus Peter, Emmanuel Charles/ Paschal Frank dk84, Abdulrahman Said, Bablas Chitembe, Rajab Rashid, Hajji Juma/Kauswa Bernard dk60, Mussa Hajji Gabi/Abubakar Segeja dk84, Waziri Junior, Jordan John/Ndaki Robert dk60 na Herbert Lukindo.