……………………………………………………………
NJOMBE
Mwanasiasa mkongwe aliyewahi kuwa Katibu mkuu wa NCCR Mageuzi,Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti Chadema na Mjumbe wa kamati ya UKAWA 2015 Juju Maltin Danda ambaye alikabidhiwa kadi ya uanachama na mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe Jasel Mwamwala may 20 mwaka huu , Leo julai 15 amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho ya kuwa mgombea ubunge wa jimbo la Njombe mjini.
Mgombea huyo anafikisha idadi ya watia nia 26 wa jimbo la Njombe mjini wanaoomba dhamana ya ya chama cha mapinduzi kupeperusha bendera ya nafasi ya ubunge katika uchaguzi mkuu hatua ambayo inaongeza ushindani zaidi na homa kwa wagombea kuelekea uchaguzi huo.
Awali akitoa maelekezo yanayopaswa kufuatwa na wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani ili kukidhi sifa ya kuingizwa kwenye mchakato wa kura za maoni katibu wa chama cha mapinduzi wilaya ya Njombe Haridi Msabaha ametoa onyo kwa watia nia ambao watakiuka kanuni na taratibu za chama ikiwemo kuanza kampeni kabla ya wakati pamoja na kutumia lugha ya matusi dhidi ya watia nia wengine ambapo anasema kufanya hivyo kunamuondolea sifa ya kupewa dhamana na chama.
Mara baada ya kukabidhiwa fomu mtia huyo akaweka bayana sababu yake ya kuomba ridhaa ya chama ya kupeperusha bendera ya chama cha mapinduzi katika jimbo la Njombe mjini ambapo amesema kuwa amechukua uamuzi huo kwasababu ni haki yake ya msingi kugombea nafasi yeyote na kudai kwamba hataweza kuongea zaidi kuhusiana na mpango wake huo kwa kuwa bado hajapewa dhamana na chama kuanza kufanya siasa.
“Nimechukua fomu ya kugombea ubunge kwa sababu ni haki yangu ya msingi na niko tayari kutekeleza ilani ya chama endapo chama changu kitanipa dhamana ya kuwa mgombea na hata kama sitachaguliwa mimi kati ya wengi waliotangaza nia”
Jimbo la Njombe mjini ndilo lenye hamasa kubwa kisiasa ikilinganishwa na majimbo mengine ambapo hadi leo julai 15 watia 9 kutoka chadema wameomba ridhaa, ACT wazalendo mmoja huku katika chama cha mapinduzi kukiwa na wagombea 26 hadi sasa.