*******************************
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
16,July
MKUU wa wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani Zainab Kawawa, ameagiza Kampuni ya Kijiko pamoja na wananchi wa Kijiji cha Kiharaka kutoliendeleza eneo hilo lenye hekari 100, mpaka watakapopewa maelekezo ya Serikalini.
Aidha ameshangazwa na Serikali ya Kijiji hicho kutoa ardhi hekari 100 kwa Kampuni hiyo, kwa lengo la kujenga nyumba za bei nafuu wakati mpaka sasa hakuna ujenzi wowote, na kwamba Kijiji uwezo wake wa kutoa ardhi mwisho hekari 50.
Kawawa alitoa kauli hiyo ,kijijini hapo alipokwenda kusikiliza kilio cha wakazi waliolalamikia kuwepo kwa zoezi la upimaji ardhi na kuwekwa mawe wakidai kwamba eneo lao tayari limepimwa, huku wananchi wakiwa na hati ya kumiliki, ambapo wanashangazwa na zoezi hilo.
Alieleza ,amepata taarifa ya mgogoro ulioanzia mwaka 2000 na 2010, kampuni ina nyaraka zinazoonyesha hati, wakati pia kwa wananchi wanaonesha hati za maeneo yao.
Baadhi ya wakazi Sharifa Salehe, AllyMan Mohamed na Marrey Abdallah wàmeshukuru kwa namna Kawawa anavyofuatilia kwa karibu sakata hilo .
“Tunaishukuru Serikali ya wilaya chini ya Mkuu wetu Zainab Kawawa kwa jitihada zake kuhusiana na mgongano huu, pia tunamuomba Rais Dkt. John Magufuli aliingilie suala letu kwani limeshakwenda Mahakamani tukashinda lakini bado tunaendelea kusumbuliwa,” alisema Sharifa.
Mmoja wa vijana wa wamiliki wa ardhi hiyo ya hekari 100 ,Marrey ameviomba vyombo vinavyofuatilia suala hilo visimamie kwa umakini ili waweze kupata haki yao ya kimsingi.