Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Raais-TAMISEMI, anayeshughulikia Afya Dkt. Dorothy Gwajima, akikagua eneo ambali lilikuwa limetengwa na Halmashauri kwaajili ya ijenzi wa Hospitali ya Wilaya.
Naibu Katibu Mkuu akikagua shughuli za Afya katika Halmashsuri ya Mlimba mkoani Morogoro wakati wa ziara yake.
********************************
Na. Atley Kuni-MOROGORO
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afya Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Dorothy Gwajima, amezisisitiza Sekretarieti za Mikoa yote nchini kujiridhisha na maeneo yaliyotengwa na Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali kabla ya kuanza ujenzi huo. Dkt Gwajima ameyasema hayo akiwa Halmashauri ya Mlimba mkoani Mrogoro katka ziara ya kikazi ya kufuatilia mpango wa Serikali wa ujenzi wa Hospitali 28 za Halmashauri zilizopewa Tsh milioni 500 kila mmoja kwenye mwqaka wa fedha 2019/20.
Katika Halmashauri hiyo Naibu Katibu Mkuu huyo, alitembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali hiyo na kubaini uwepo wa miinuko mikali na hivyo kuielekeza Halmashauri hiyo kufanya utaratibu wa kubadilisha eneo hilo na kuchagua lenye nafuu ili kuepuka gharama kubwa za kudhibti miinuko na mabonde hayo yanayoweza pia kuathiri mchakato wa uendeshaji wa huduma.
“Mkumbuke kuwa eneo hili litatumiwa na wagonjwa wa aina mbalimbali hivyo lazima liwe rafiki na siyo liwe chanzo cha kero na changamoto kwa wagonjwa, watoa huduma na kwa bajeti ya Serikali, hivyo tafuteni eneo mbadala. Na nyie wataalamu wa afya mliopo Halmashauri simameni katika nafasi zenu” amesema Dkt Gwajima.
Dkt. Gwajima ametumia fursa hiyo kuzitahadharisha Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri zingine nchini kuwa zishirikiane katika kuhakiki maeneo husika na kuwepo na muhtasari wa makubaliano kuwa eneo hilo limehakikiwa na kukubalika kuwa ni sahihi na ngazi zote yaani Halmashauri na Mkoa.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt Kusire Ukio amesema hakubaliani na kwamba huo ndio mwanzo wakuzalisha gharama, amesema, mtakuja kujenga hapa Hospitali moja na nusu wakati wenzenu kwa kiasi hicho hicho wameweza kukamilisha majengo yaliyokusudiwa huku akitoa ahadi mbele ya Naibu Katibu Mkuu, na kumuhakikishia kufuatilia kwa karibu na kutoka na majawabu sahihi juu ya nini kifanyike na ujenzi wa Hospitali uendelee na kutoa ahadi ya kutoa taarifa Ofisi ya Rais TAMISEMI ndani ya juma moja toka tarehe ya ziara hiyo.
Akionesha kukiri mapungufu hayo Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo Dkt. Christina Guvert alisema, yeye pamoja na timu ya wataalamu amepokea na ameahidi kufanya utekelezaji ndani ya siku 14 na kisha kuwasilisha taarifa kwa Mganga Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kuiwasilisha Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI, imekwishatoa kiasi cha milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali Mpya za Halmashauri za Wilaya 28 kwa mwaka wa fedha 2019/20 ikiwa ni awamu ya pili ya mkakati wa ujewa Hospitali hizi ulioanza na awamu ya kwanza ya ujenzi wa Hospitali 67 mwaka wa fedha 2018/19 ambapo tayari majngo ya Hospitali 53 yameanza kutumika.
Hivi sasa wataalamu kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Sekretarieti za Mikoa yote na wadau wanaendelea na zoezi la ufatiliaji wa karibu ili kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unafanyika kwa tija na kudhibiti changamoto zisizo za lazima.