…………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imesema itahakikisha miradi yote ya serikali inayosimamia inatekelezwa kwa viwango vyenye ubora wa hali ya juu na kwa gharama nafuu ikilinganishwa na taasisi nyingine za ujenzi.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Mtendaji Mkuu wa TBA, Wencelous Kizaba katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba Jiji Dar es salaam baada ya TBA kushika nafasi ya kwanza ya utoaji huduma bora katika kipengele kinachojumuisha Wizara, Mamlaka za Serikali na Taasisi zingine za serikali.
Amesema Wakala huo umekuwa ukisimamia ujenzi wa miradi mbalimbali ya serikali ikiwemo ujenzi wa rada katika viwanja mbalimbali vya ndege, ofisi za halmashauri, hospitali na mradi wa nyumba za makazi Magomeni kota wanaamini hadi kufikia Oktoba mwaka huu miradi mingi itakuwa imekamilika na kukabidhiwa.
Ameeleza kukabidhiwa kwa Tuzo hiyo kunawapa nguvu zaidi ya kuendelea kutekeleza miradi mingine kwa ubunifu na weledi mkubwa.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa TBA, Renatus Sona amewashukuru watu na wadau wote waliotembea banda la TBA katika maonyesho hayo ya 44 na kwamba tuzo hiyo inaashiria wamefanya kazi nzuri na kutekeleza miradi kwa umakini.