Viongozi na baadhi ya watumishi wa Makumbusho ya Taifa wakimsikiliza Afisa Utalii wa Jiji Benard Tahondi akieleza kuhusu chimbuko la mji wa Dar es Salaam ndani ya jengo la Old Boma jijini Dar es Salaam.
Viongozi na baadhi ya viongozi wa Makumbusho ya Taifa wakitembea mbele ya jengo la St, Joseph Cathedral halimo pichani walipotembelea majengo ya kihistoria yaliko jijini Dar es Salaam.Viongozi na baadhi ya watumishi wa Makumbusho ya Taifa wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa wa utalii wa jiji mbele ya jengo mojawapo linalohifadhiwa la Karimjee.
*************************************
Na Mwandishi Wetu
Viongo na baadhi ya watumishi wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania wametembelea maeneo na majengo ya kihistoria yaliyoko kwenye eneo la hifadhi la jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kutalii, kujifunza na kuyaona baadhi ya majengo ya malikale yaliyokasimishwa kwa Taasisi hiyo.
Katika ziara hiyo iliyoongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga waliweza kutembelea majengo zaidi ya 20 ambayo yamehifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa anasema kuwa uhifadhi wa majengo na maeneo ya kihistoria ni muhimu katika kutunza urithi wa asili na historia ya nchi yetu.
Dkt. Lwoga amesema kuwa Makumbusho ya Taifa imekasimishwa zaidi ya majengo 40 katika jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa ushauri wa kitaalamu wa uhifadhi na utunzaji wa maeneo/majengo hayo.
“Haya majengo yamejengwa siku nyingi lakini yana maana kubwa kwa urithi wa nchi yetu kwa kizazi cha sasa na kijacho, hivyo bila kuhifadhiwa tutapoteza historia na urithi wa nchi yetu” alisema Dkt Lwoga.
Baadhi ya maeneo na majengo yaliyotembelewa ambayo yako chini ya jiji la Dar es Salaam ni pamoja na jengo la zamani kuliko yote jijini Dar es Salaam lililojengwa mwaka 1866 la Old Boma, jengo la Kanisa katoriki la St Joseph Cathedral, jengo la shule ya Sekondari St, Joseph, jengo la White fathers (Atman), jengo la Posta ya zamani, jengo la Karimjee Jivanjee, na bustani ya kumbukumbu ya vita (War memorial garden) yaliyo kandokando ya Barabara ya Samora.
Mengine ni jengo la Kanisa la Lutherani la Azania Front, jengo la Mahakama ya Rufaa, jengo la Mahakama Kuu, jengo la Karimjee, jengo la hospitali ya Ocean Road, Bustani ya jiji, mnara wa askari na mengineyo.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Afisa Utalii wa Jiji, Daniel Kobelo amewashukuru viongozi wa Makumbusho ya Taifa kwa kutembelea maeneo na majengo ya kihistoria na kusema kuwa ilikuwa fursa nzuri kwao kupata uzoefu na utaalamu wa kimakumbusho.
“Kazi hii ni kweli tunaifanya lakini tumejifunza mambo mengi kutoka kwenu siku ya leo kwa sababu ninyi ni wataalam wa uhifadhi wa maeneo ya kihistoria,” alisema Bw. Kobelo.
Amesema uhifadhi ni jamba gumu kufanyika na taasisi moja hivyo, ameomba ushirikiano wa wadau mbalimbali.
“Hii inaweza ikawa mwanzo mzuri wa ushirikiano wa Jiji na Makumbusho na wadau wengine wanaweza kujitokeza katika kuhifadhi maeneo haya ya kihistoria na urithi kwa nchi yetu.