Balozi wa Ujerumani Tanzania Mh. Regina Hess akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika banda la Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga & Mloganzila) katika maonyesho ya 44 ya biashara yanayoendelea katika viwanja vya SABASABA.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Muhimbili Bw. Aminiel Aligesha akizungumzia kuhusu huduma mbalimbali za afya zinazotolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Garvin Kweka akimuelezea Balozi Hess namna ya kumuhudumia mgonjwa mwenye matatizo ya figo.
Balozi Regina Hess (kulia) kizungumza wakati alipotembelea banda la Muhimbili (Upanga na Mloganzila) kwa lengo la kujionea utoaji wa huduma, katikati ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Bw. Aminiel Aligaesha na kushoto ni Muuguzi Lenick Chaula.
***************************
Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Mh. Regine Hess ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga & Mloganzila) kwa kuanzisha huduma mbalimbali za kibingwa ambazo zimesaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Pongezi hizo zimetolewa na Balozi huyo alipotembelea banda la Muhimbili katika maonyesho ya 44 biashara yanayoendelea katika viwanja vya SABASABA.
Akizungumza wakati wa ziara yake Balozi Hess amesema uwepo wa huduma za kibingwa ni dhahiri kuwa huduma za afya nchini zimeimarika kwa kiwango kikubwa.
Awali Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Hospitali ya Taifa Muhimbili Bw. Aminiel Aligaesha amemueleza Balozi huyo kuwa katika kipindi cha miaka mitano 2015-2020, Muhimbili imefanikiwa kuanzisha huduma mbalimbali za kibingwa ikiwemo upandikizaji wa figo (kidney transplant), upandikizaji wa vifaa vya kusaidia kusikia (cochlear implant), huduma ya kuvunja mawe kwenye figo kwa kutumia teknolojia ya kisasa (extracorporeal shock wave lithotripsy ESWL), upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo pamoja tiba radiolojia.
Awali kabla ya kuanzishwa kwa huduma hizi ililazimu wagonjwa wenye matatizo haya kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, hivyo hatua hii imeleta afueni kwa Watanzania.
Katika hatua nyingine, Balozi Hess ameipongeza Muhimbili kwa jitihada za kupambana na Covid19 kwa kuzalisha vazi kinga (PPE) ambalo lilitoa nafasi ya watoa huduma kutoa huduma kwa usalama.