Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Brigedia Jenerali Charles Mbuge akitia saini kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili Chuo kikuu Mzumbe.Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Lughano Kusiluka akizungumza na viongozi (hawapo pichani) wa JKT mara baada ya kuwasili Chuoni hapo kukagua maendeleo ya miradi ya Ujenzi inayojengwa na Kampuni ya Suma JKT.Makamu Mkuu wa Chuo Prof.Lughano Kusiluka (Mwenye suti) akifurahia jambo na viongozi wa JKT eneo zinapojengwa Hosteli za Wanafunzi Kampasi Kuu Morogoro– Maekani. Menejimenti ya Chuo Kikuu Mzumbe wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa JKT baada ya kuhitimisha ziara ya ukaguzi wa jengo la madarasa na kumbi za mihadhara Kampasi Kuu Morogoro.
*******************************
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Brigedia Jenerali Charles Mbuge amefanya ziara ya kukagua miradi miwili ya ujenzi ya Chuo kikuu Mzumbe inayojengwa na Kampuni ya SUMA JKT “M/S SUMA JKT Construction Company Limited” na kuahidi kusimamia kwa karibu miradi hiyo ili kukamilika kwa wakati.
Akiwa ameambatana na viongozi wa ngazi za juu wa Jeshi hilo, walipokelewa na Menejimenti ya Chuo Kikuu Mzumbe, na kukagua hatua za ujenzi wa hosteli za Wanafunzi ambao umekamilika kwa asilimia 85% pamoja ujenzi wa madarasa na kumbi za mihadhara ambao umekamilika kwa asiliamia 55%.
Akimkaribisha Mkuu huyo wa JKT, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Lughano Kusiluka, amepongeza ushirikiano mzuri uliopo katika utendaji kati ya Chuo Kikuu Mzumbe na JKT, na kuanisha hatua za ujenzi wa miradi hiyo ya maendeleo, changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji hususani kwenye ujenzi wa Hosteli za wanafunzi; na kumwomba Mkuu huyo wa JKT kusaidia miradi hiyo kukamilika kwa wakati, ili majengo hayo yaanze kutumika kwa mwaka wa masomo 2019/20 kama ilivyodhamira ya Serikali.
Akizungumza mara baada ya kukagua miradi hiyo, Brigedia Jenerali Charles Mbuge, amekipongeza Chuo kikuu Mzumbe kwa kutumia fedha zake za ndani kwenye miradi ya maendeleo, na kuahidi kuifuatilia miradi hiyo kwa ukaribu na kuhakikisha inakamilika kwa wakati kama ilivyokubalika baina ya Mshitiri na Mkandarasi.
Mradi wa ujenzi wa hosteli umefadhiliwa na Serikali kwa jumla ya shilingi bilioni 6.5 wakati mradi wa ujenzi wa madarasa na kumbi za mihadhara unafadhiliwa na fedha za ndani za Chuo Kikuu Mzumbe kwa Shilingi Bil 3.11