Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Isack Kamwelwe, akizungumza na wananchi (hawapo pichani) waliohudhuria hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara ya njia nne ya mzunguko ya jiji la Dodoma (km 112.3), kiwango cha lami.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Isack Kamwelwe, na viongozi wengine wa meza kuu wakifuatilia utiaji saini makubaliano ya ujenzi wa barabara ya njia nne ya mzunguko ya jiji la Dodoma (km 112.3), kiwango cha lami kati ya Wakala wa Barabara (TANROADS) na wawakilishi wa mkandarasi Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Isack Kamwelwe, na viongozi wengine wa meza kuu wakifuatilia utiaji saini makubaliano ya ujenzi wa barabara ya njia nne ya mzunguko ya jiji la Dodoma (km 112.3), kiwango cha lami kati ya Wakala wa Barabara (TANROADS) na wawakilishi wa mkandarasi AVIC INTL Project Engineering Company, jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Patrick Mfugale na Mkandarasi kutoka Kampuni ya AVIC INTL Project Engineering Company, wakionesha hati ya makubaliano ya ujenzi wa barabara ya mzunguko sehemu ya Ihumwa Dry Port – Matumbulu – Nala (km 60), jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Isack Kamwelwe, na viongozi wengine wa meza kuu wakishuhudia ubadilishanaji wa hati ya makubaliano ya ujenzi wa barabara ya njia nne ya mzunguko ya jiji la Dodoma (km 112.3), kiwango cha lami kati ya Wakala wa Barabara (TANROADS) na mwakilishi wa mkandarasi Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), jijini Dodoma.
Baadhi ya wananchi wakifuatilia hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara ya njia nne ya mzunguko ya jiji la Dodoma (km 112.3), kiwango cha lami.
************************
Serikali imesaini mikataba miwili ya ujenzi wa barabara ya mzunguko wa jiji la dodoma kwa kiwango cha lami ya njia nne yenye urefu wa kilometa 112.3 ili kupunguza msongamano katika jiji hilo.
Mikataba iliyosainiwa ni baina ya Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa niaba ya Serikali na wakandarasi wawili Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na AVIC INTL Project Engineering Company walioshinda zabuni ambao watajenga barabara hiyo kwa kipindi cha miezi 36.
Mkandarasi Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), atajenga kilometa 52.3 kuanzia Nala – Veyula – Mtumba – Ihumwa Dry Port na mkandarsi AVIC INTL Project Engineering Company atajenga kilometa 60 itakayoanzia Ihumwa Dry Port – Matumbulu hadi Nala.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Isack Kamwelwe, amewataka wakandarasi hao kukamilisha ujenzi huo kwa viwango ikiwezakana kabla ya wakati uliopangwa na kuwataka wananchi watakaopata fursa katika ujenzi huo kufanya kazi kwa bidii na uadilifu.
Amemtaka Mkurugenzi wa jiji la Dodoma kuangalia namna ya kuwawezesha wawekezaji kupata maeneo kwa bei nafuu katika maeneo yanayopitiwa na mradi huo ili kuwekeza na kukuza uchumi wa jiji.
“Mkurugenzi hakikisha wawekezaji wote watakaohitaji kuwekeza katika maeneo yanayopitiwa na mradi huu wanapata maeneo hayo kwa haraka ili waweze kuhamasisha mzunguko wa uchumi katika jiji hili na kutoa huduma kwa wasafiri na wasafirishaji watakaotumia barabara hiyo inayopita nje ya jiji la Dodoma”, amesisitiza Waziri Kamwelwe.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Patrick Mfugale, amesema zaidi ya shilingi bilioni 221.7 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo.
Barabara ya njia nne ya mzunguko ya jiji la Dodoma inatarajiwa kupunguza foleni katikati ya jiji na kuunganisha kwa urahisi barabara kuu zinazounganisha jiji hilo na mikoa jirani ya Singida, Manyara, Morogoro na Iringa.