*****************************
Wanasheria Vishoka ‘Bush Lawyers’ wapigwa marufuku kutoa Huduma ya Msaada wa Kisheria kwa wananchi.
Marufuku hiyo imetolewa leo na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria ndugu Amon Mpanju wakati akizindua Kamati ya Uratibu wa Huduma ya Msaada wa Kisheria Wilayani Bukoba Mkoa wa Kagera.
“Tumerasimisha huduma hii ili kuwaepusha wananchi hasa Wanawake, Watoto, Wazee na Walemavu kukumbana na matapeli katika harakati za kuitafuta na kuifikia haki kwa wakati. Bush Lawyers ni matapeli kama matapeli wengine kwani hatuwatambuliki Kisheria.” Amesisitiza Mpanju.
Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo ameitaka Kamati ya Uratibu wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kuhakikisha Taasisi zote 15 ambazo hazijasajiliwa na zinatoa huduma ya msaada ekisheria zinasajiriwa ili kukidhi vigezo vya utoaji huduma hiyo kwa wananchi kwa mujibu wa Sheria Na 1 ya Mwaka 2017.
“Nawapa wiki mbili tu kuhakikisha mmezisajiri taasisi zote mkoani Kagera zinazotoa huduma kwani zinamsaada mkubwa kwa wananchi wanyonge kuifikia haki.” Ameagiza Mpanju.
Hata hivyo, Amon Mpanju ameenda mbali zaidi kwa kueleza umuhimu wa watoa huduma ya msaada wa kisheria na Wasaidizi kuwa wanasaidia kutatua migogoro katika jamii bila kufika mahakamani jambo linalochangia kupunguza mrundikano wa mashauri mahakamani hivyo, kusaidia wananchi kuwa na muda wa kutosha kufanya kazi za uzalishaji mali unaochangia kukuza pato la Taifa.
Uzinduzi wa Kamati hii ni mfurulizo wa uundwaji wa Kamati za Uratibu wa Huduma ya Msaada wa Kisheria katika ngazi za Mkoa kwa mujibu wa Sheria ya Msaada wa Kisheria Na. 1 ya Mwaka 2017 ambayo imeweka mfumo wa uratibu wa watoa huduma za msaada wa kisheria nchini. Mfumo huu unaanzia kwenye ngazi ya Serikali Kuu hadi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.