Mwenyekiti wa Kamati ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Takwimu ya Jaji Mkuu ,Mhe. Shaaban Lila (katikati) ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, akizungumza jambo jana wakati akifungua kikao cha kamati hiyo kwenye ukumbi wa mkutano wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi uliopo Jijini Dar es Salaam.
Katibu Kamati ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Takwimu, ambaye pia ni Mkurugenzi wa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Enock Kalege akitoa taarifa ya maendeleo ya teknolojia hiyo.
……………………………………………………………………………..
Na Magreth Kinabo – Mahakama
Mwenyekiti wa Kamati ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Takwimu ya Jaji Mkuu, Mhe. Shaaban Lila amewataka wajumbe wa kamati hiyo kutoa uzoefu wao kuhusu matumizi ya teknolojia na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika eneo hilo.
Akizungumza jana wakati akifungua kikao cha kamati hiyo cha siku mbili kilichofanyika kwenye ukumbi wa mkutano wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi uliopo Jijini Dar es Salaam, Jaji Lila, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, alisema teknolojia hiyo imeanza kutumika mahakamani na wana majukumu tisa ya kuyafanyia kazi.
‘‘Tutumie kikao hiki kubadilishana uzoefu na kuzitafutia ufumbuzi changamoto tunazokabiliana nazo katika matumizi ya TEHAMA ukitaka kutatua tatizo ni lazima uliweke bayana na kulitafutia ufumbuzi, ’’ alisema Mwenyekiti huyo.
Lila aliongeza kwamba kamati hiyo imepewa majukumu mbalimbali ya kuyatekeleza ili kuhakikisha eneo la TEHAMA linatekelezwa ipasavyo, hivyo aliwataka wajumbe hao kutoa ushauri wa kuendelea kuboresha eneo hilo.
Alifafanua kuwa mifumo ya TEHAMA iendelee kuboreshwa iwe ya manufaa kwa wananchi na Mahakama pia kuwataka wajumbe wa kikao hicho kuyataja maeneo yanayotakiwa kuboreshwa.
Kwa upande wake Katibu wa kamati hiyo, ambaye pia Mkurugenzi wa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Enock Kalege akitoa taarifa ya maendeleo ya teknolojia hiyo, alisema imeleta matokeo chanya katika shughuli mbalimbali za Mahakama licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto kama vile rasilimali fedha na watu kwa ajili ya kuendelea kulitekeleza jukumu husika.
Kalege alisema kwamba teknolojia hiyo pia inasaidia kuwa na takwimu sahihi kama vile vifaa vya TEHAMA ili kuweza kuboresha na kupanga mipango ya sasa na baadae kwa faida ya Mahakama.
‘‘Tumefanikiwa kukamilisha jukumu hili la TEHAMA kwa asilimia 71 kupitia miradi ya uwekezaji kwenye eneo hili, na tunaendelea kutekeleza asilimia 29 iliyobakia,’’ alisisitiza.
Akizungumzia kuhusu eneo hilo, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma alisema kwa upande wa kufungua mashauri kwa njia ya Mahakama Mtandao limeendelea kutekelezwa kama ilivyoagizwa na Jaji Mkuu wa Tanzania.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru alisema ili kuhakikisha teknolojia hiyo inaendelea kurahisisha huduma ya utoaji haki na kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli tofauti za Mahakama ni vema watumishi wakaendelea kujengewa uwezo na kubadili mitazamo yao.