……………………………………………………………………………
NA MWAMVUA MWINYI ,PWANI
BAADHI ya wakulima kijiji cha Kitonga na Kidogozero ,kata ya Vigwaza ,Chalinze mkoani Pwani ,wamelalamikia tabia ya wafugaji kuingiza mifugo yao kiholela katika mashamba yao na kusababisha kula mazao na kuwasababishia hasara .
Wamesema vitendo hivyo vimekithiri hivyo wameomba uongozi wa kata ,wilaya na mkoa kuendelea kusimamia kero hiyo ili waishi kwa amani .
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)tawi la Kidogozero,Vera Sultan Mindu alisema ,tatizo hilo walishawahi kulitolea taarifa wilaya na mkoa na kijiji kilijiwekea sheria ndogondogo lakini wafugaji wamekuwa wakiingiza mifugo kiholela na kunyanyasa wakulima hata wakiwa wanajaribu kuwaeleza makosa yao .
Akizungumza wakati akitoa kero hiyo wakati diwani anaemaliza muda wake ,Mohsin Bharwani alipokwenda kuwaaga rasmi na kutoa taarifa ya utekelezaji ya kijiji na kata ,Vera alisema wafugaji hawaogopi hata kushtakiwa polisi hali ambayo inawakatisha tamaa wakulima .
“;Wapo wafugaji ambao wamenunua maeneo kijijini hapo lakini ni ya kujenga na kuishi na sio kufuga ,unakuta wao wanafuga na kero zaidi ipo kwa wafugaji wanaoitana kutoka maeneo ya nje na kijiji hicho “; Vera alifafanua .
Bharwani alifanya mkutano wa aina hiyo pia kijiji cha Kitonga ambako ,mwenyekiti wa kijiji hicho ,Enock Mhingo ,alisema wamechoshwa na wafugaji ,wanaingiza mifugo katika mashamba .
” Kuna changamoto nyingine ya barabara ya Ruvu -Kitonga kutopitika vizuri hasa nyakati za mvua ya masika,tuna mahitaji pia ya umaliziaji wa vyumba vya madarasa matatu shule ya msingi Kitonga na zahanati “alisema Mhingo.
Nae mfugaji anaeishi kijiji cha Kitonga almaarufu Lake ,alieleza ni kweli tatizo lipo ,na kama serikali kupitia kamati za maridhiano wakisimama kidete tatizo litaisha.
Alisema ,kuanzia sasa watakuwa wakiwakemea hasa wafugaji wanaotoka nje ya kijiji ili waishi kwa amani na wakulima .
Diwani anaemaliza muda Vigwaza ,Mohsin alitoa wiki moja kwa TAKUKURU Chalinze iende ikachunguze tatizo kijiji cha Kitonga ambacho sheria ndogo zipo lakini wafugaji wanaonekana kuwa na nguvu .
Mohsin ,aliomba viongozi wa kijiji kuacha kupindisha sheria ndogondogo walizojiwekea ,na kulinda kundi lenye pesa ,kwa kufanya hivyo wanasababisha kundi linalonyimwa haki kuishi bila raha na kwa hasara .
” Kuweni makini viongozi wenzangu wa vijiji ,simamieni wananchi hawa kwa haki ili kulinda amani na waishi kwa upendo pasipo chuki na migongano ,:!alisisitiza Mohsin .
Mohsin alichangia mifuko ya saruji 100 na matofali 2,000 katika ujenzi wa shule ya msingi Kitonga na mifuko ya saruji 50 itakayoelekezwa ujenzi wa zahanati.