Home Makala TAEC YATOA ELIMU JUU YA SABABU UPIMAJI WA MIONZI KWENYE MNYORORO WA...

TAEC YATOA ELIMU JUU YA SABABU UPIMAJI WA MIONZI KWENYE MNYORORO WA BIDHA, MAONESHO YA  SABASABA, JIJINI DAR ES SALAAM

0

Aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya TAEC iliyokwisha muda wake Dkt. Furaha Mramba, akisaini kitabu cha wageni katika banda la Tume ya Nguvu za Atomic katika viwanja vya Sabasaba vya Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam. Aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya TAEC iliyokwisha muda wake Dkt. Furaha Mramba akizungumza jambo na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania Bw.Peter Ngamilo, katika banda la Tume ya Nguvu za Atomi katika viwanja vya Sabasaba vya Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.

*************************************

Nchi ya Tanzania ina mamlaka mbalimbali zenye kazi za udhibiti kwenye mnyororo wa bidhaa ili kuhakikisha ubora  na usalama wa bidhaa dhidi ya sumu, kemikali, ubora mdogo na mionzi ili kuwalinda  watanzania  wanaotumia bidhaa zozote  zinaoingizwa  nchini.

Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) ni mamlaka moja wapo ya udhibiti   inayojishughulisha na kulinda usalama wa watanzania dhidi ya mionzi katika mnyororo wa bidhaa hapa nchini, TAEC imeundwa kwa Sheria  ya Nguvu za Atomiki Na. 7 ya Mwaka 2003 (Atomic Energy Act No.7 of 2003) inayoipa TAEC mamlaka ya kudhibiti matumizi salama ya mionzi na kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia nyuklia nchini ili kulinda wananchi na mazingira dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi. Teknolojia ya nyuklia inatumika katika sekta mbalimbali hapa nchini zenye manufaa ya kiuchumi na kijamii kama vile Afya, Kilimo, Ufugaji Viwanda, Maji,Utafiti na ujenzi.

Hayo yamesema na Bw. Peter Ngamilo Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania TAEC wakati akizungumza na mtandao wa Fullshangweblog katika maonesho ya biashara ya kimataifa ya TANTRADE yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam.

Bw. Peter Ngamilo amesema TAEC imekuwa ikifanya kazi  ya kupima mionzi katika mnyororo wa bidhaa mbali mbali zinazoingia nchini na kusafirirshwa nje ya nchi ili kuhakikisha wananchi wanaotumia bidhaa hizo wanakuwa salama, Mionzi ni hatari sana ikiingia katika mnyororo wa bidhaa   kwa sababu inatoa nishati  toka katika kiini cha atomu ambayo haiwezi kuharibiwa kwa aina yoyote ile. Viasili hivi vya mionzi vinaweza kuathiri afya ya binadamu na wanyama,  hivyo, zipo sababu nyingi za kupima mionzi huku lengo kuu ni kuhakikisha bidhaa  zinazotumiwa na Watanzania hazina mionzi na hivyo kuwa salama kwa matumizi ya kawaida.

Ameongeza kuwa sababu nyingine ni  kulinda soko la bidhaa zetu zinazokwenda nje ya nchi kutokana na sababu kwamba kumekuwepo na matukio mbalimbali ya vita za kiuchumi yanayoendelea katika nchi mbalimbali duniani, hivyo kwa kupima bidhaa zetu zinazokwenda nje tunaongeza wigo wa kiusalama wa bidhaa zetu  ili isije ikatokea watu/wafanyabiashara wenye nia ovu na nchi yetu wakaweka viasili vya mionzi kwenye bidhaa zetu hivyo ikaonekana bidhaa kutoka Tanzania zina mionzi na kisha kupelekea kutokubalika kwa bidhaa za Tanzania katika masoko ya nje.

“Zipo bidhaa nyingi za chakula zinazoingia nchini ambazo bila kupima na kujua viwango salama vya mionzi kunaweza kuhatarisha afya za watanzania wengi, jambo ambalo hupelekea kupima mionzi kila bidhaa ya vyakula  inayoingia nchini au kusafirishwa nje ya nchi na wafanyabiashara wa ndani ya nchi” Amesema Peter Ngamilo..

Ameongeza kuwa pia kutokana na baadhi ya watu wasio waaminifu kufanya mambo kinyume na sheria na utaratibu unaoweza kupelekea usafirishaji usio rasmi wa vyanzo vya mionzi (illicit trafficking) kwa njia ya magendo  unaweza kusababisha uchafuzi  mkubwa kwenye mnyoroo  wa bidhaa  na mazingira hivyo upimaji unatoa viashiria endapo kutakuwa na uchafuzi ili  hatua stahiki zichukuliwe kwa lengo la kulinda afya ya  binadamu.

Bw. Ngamilo alieleza sababu nyingine ya kupima ni kuendelea kuangalia usalama kwani kuna mionzi asili kwenye udongo na katika mazingira tunayoishi kama madini ya urani yaliyopo maeneo mbalimbali nchini  ni moja ya sababu muhimu inayoifanya TAEC kupima viasili vya mionzi kwenye bidhaa ili kuondoa hali ya hatarishi inayoweza kujitokeza.

“Matakwa ya kisheria yanahitaji Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania kupima mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa kama ilivyoahinishwa kwenye Sheria Na. 7 ya Mwaka 2003, ambapo inaeleza kuwa ni wajibu wa Serikali kulinda wananchi wake, hivyo imechukua hatua za kulinda mnyororo mzima wa chakula ili wananchi wake wawe salama” Amesema Ngamilo.

Ngamilo aliendelea kusema vile vile kutokana na makubaliano na ushirikiano ili kutimiza matakwa ya  Sheria za taasisi za kimataifa na  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo  Tanzania ni mmoja wa wanachama, Sheria ya Afya Duniani (WHO), Shirika la Kilimo na Afya Duniani (FAO) na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) katika kuhakikisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia hivyo kutokana na uanachama huo yapo makubaliano ya  nchi wanachama kupima vyakula vitokavyo na viingiavyo katika nchi wanachama ili kubaini kama kuna  vimelea vya mionzi katika kukidhi makubaliano na mikataba ya kimataifa kama nchi mwanachama kati ya Tanzania na Shirika hilo.

Amesisitiza kuwa ikumbukwe pia bidhaa zinazongia nchini zinapaswa kupimwa na kuona kama kuna vimelea vya mionzi kwani, hii imetokana na ajali mbalimbali za milipuko ya vinu vya  kinyuklia kama vile ajali ya kinu cha nyuklia iliyotokea tarehe 26 Aprili, 1986 nchini Ukraine ambayo ilisababisha mionzi kuingia kwenye mazingira, anga na maji hivyo nchi zote ambazo ni wanachama wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) kufanya makubaliano ya kupima mionzi kwa bidhaa zote zinakazokuwa zinatoka na kuingia katika nchi wanachama. Vilevile ajali ya kinu cha nyuklia iliyotokea kule Japan Fukushima, Daiichi tarehe 11 Machi, 2011 nayo ni moja ya sababu za nchi wanachama kuona kuna umuhimu wa kuendelea kupima mionzi katika mnyororo wa bidhaa.

Ameongeza kuwa katika kufanikisha zoezi hili kumekuwa na gharama zinazohusisha uendeshaji na utoaji wa huduma hii, hivyo TAEC imekuwa ikitoza  gharama nafuu na rafiki kwa wateja ili kufanikisha upimaji wa mionzi katika mnyororo wa bidha, Utafiti uliofanywa na Taasisi ya utafiti ya Torita iliyofanya utafiti juu ya gharama kamili katika uwezeshaji wa uendelezaji wa zao la tumbaku nchini ulibaini kuwa TAEC ina tozo za gharama ya chini katika zoezi zima la upimaji wa mionzi katika mnyororo wa bidhaa ukilinganisha na gharama za upimaji wa bidhaa hizo hizo katika taasisi nyingine zinazofanya udhibiti katika bidhaa mbali mbali hapa nchini ambapo  TAEC hutumia malipo yanayolipwa kwa ajili ya kuchukulia sampuli zinazopimwa, gharama za kununua vifungasihio vya sampuli, gharama za kusafirisha kwenda maabara, gharama za kuandaa sampuli kabla ya kuzipima.

Gharama nyingine ni pamoja na gharama za umeme, maji, kemimkali, sampuli rejea mbalimbali, gharama za ununuzi na uzalishaji wa hewa baridi ya Naitrojeni (Liquid Nitrogen Gas) ambayo hutumika kupoozea vifaa ndani ya maabara pia gharama zingine ni za  utunzaji wa sampuli kwa kipindi cha miezi mitatu kama Sheria inavyoelekeza hii ikienda sambamba na gharama za kuharibu sampuli muda wa ukomo wa utunzaji wa sampuli unapofikia.

Amezitaja na kueleza kuwa gharama ndogo zinazoanzia  kiasi cha shilingi elfu 35,000 hutumika katika kupima sampuli mbalimbali zinazoletwa maabara na hatimaye kufanya TAEC kuwa taasisi namba moja katika kutoza gharama ndogo katika utekelezaji wa majukumu yake ya udhibiti ili kulinda wafanyakazi, wagonjwa, mazingira na wananchi kwa ujumla wake dhidi ya madhara hatari yanayoweza kusababishwa na mionzi.