……………………………………………………………………………
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deo Ndejembi amesema Rais Dk John Magufuli ataongoza kwa kura za Urais kwenye Wilaya ya Kongwa kulinganisha na wagombea wengine.
DC Ndejembi ameyasema hayo katika ziara yake na Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo ya kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali ikiwemo Nyumba za Walimu, Shule za Msingi na Sekondari, Miradi ya Maji, Kituo cha Afya na Kituo cha Polisi ambayo yote imegharimu kiasi cha Sh Bilioni 1.7. ” Wilaya ya Kongwa tayari tumeshaamua kuwa Rais Magufuli hana mpinzani na hata kwenye Ubunge hapana shaka Spika Ndugai atapita bila kupingwa.
Amesema ni wazi macho yao yamejionea kazi kubwa iliyofanywa na Rais Magufuli kwenye wilaya yao ndani ya kipindi cha miaka mitano na kuwataka wananchi wa Kongwa na watanzania kwa ujumla kumpigia kura nyingi za ndio Rais Magufuli ili aendelee na kazi ya kuwatumikia watanzania na kuwaletea maendeleo.
Amesema ziara aliyoifanya ilikua ni kukagua miradi mikubwa na midogo inayotekelezwa na serikali kwa kipindi chote cha miaka mitano wilayani hapo ikiwemo miradi ya Vituo vya Afya vya Kisasa vya Mkoka na Mbande pamoja na miradi ya Elimu.
Amesema licha ya kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika kutekeleza miradi mikubwa ya kitaifa lakini bado Wilaya ya Kongwa kila Kata imeguswa zikiwemo Kata za Makawa, Zoisa na Kata ya Mkoka ambapo kote huko serikali iko kazini kuwaletea maendeleo wananchi wake.
” Tumeongona na Wakuu wa Idara kwenye Halmashauri yetu na Kamati ya Siasa kwa kuwa hawa ndio hasa wasimamizi wa Ilani na wanatukagua ili wapate kutusemea vizuri huko kwa wananchi juu ya mambo makubwa yanayofanywa na serikali yao.
Tumeridhishwa na maendeleo ya ujenzi ingawa nimetoa maagizo kwa DMO kuhakikisha Kituo cha Afya Mkoka kinafanyiwa maboresho kwenye milango kwa sababu sijaridhika nayo, nimetoa siku tatu wawe wameshaitoa ile milango ili itengenezwe upya,” Amesema DC Ndejembi.
Amesema mambo aliyoyafanya Rais Magufuli ni makubwa kulinganisha na muda wa miaka minne aliyokaa madarakani.