Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Uondoshaji wa Mashauri ya Jinai ambaye pia ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Sharmillah Sarwatt (kushoto) na Katibu wa kikao hicho Naibu Msajili Mkuu Mwandamizi wa Mahakama kuu ya Tanzania Masijala Kuu Mhe Messe Chaba (kulia).
Mkurugenzi wa Menejimenti ya Usimamizi wa Mashauri Mahakama ya Tanzania, Mhe. Deusdedith Kamugisha akitoa taarifa leo ya uendeshaji wa mashauri ya jinai katika kipindi cha Januari, mwaka huu hadi Julai Moi, mwaka huu kwenye kikao kazi cha robo mwaka ya pili ya mwaka wa kimahakama cha mwaka huu kilichohusisha wadau wa Haki Jinai.
Mwakilishi kutoka katika ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), ambayo imewakilishwa na Naibu Kamishna wa Polisi. Bw.Saleh Ambika akifafanua jambo.
Kamishna Msaidizi wa Magereza, Bw,Willington Kamuhuza,(kushoto) akizungumza jambo kwenye kikao hicho. (Kulia ) ni Mkurugenzi wa Menejimenti ya Usimamizi wa Mashauri Mahakama ya Tanzania, Mhe. Deusdedith Kamugisha.
( PICHA NA MAGRETH KINABO – MAHAKAMA)
…………………………………………………………………
Na Magreth Kinabo na Innocent Kansha – Mahakama
Jumla ya mashauri ya jinai 24,698 yalifunguliwa katika ngazi zote za Mahakama nchini nzima isipokuwa Mahakama za Mwanzo kati ya hayo 25,950 yalisikilizwa sawa na asilimia 105.06 ya mashauri yote yaliyofunguliwa katika kipindi cha Januari hadi Julai Mosi, mwaka huu.
Akizungumza wakati akitoa taarifa hiyo leo ya uendeshaji wa mashauri hayo katika kipindi hicho, kwenye kikao kazi cha robo mwaka ya pili ya mwaka wa kimahakama cha mwaka huu kilichohusisha wadau wa Kamati ya Kitaifa ya Haki Jinai.
Mkurugenzi wa Menejimenti ya Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Deusdedith Kamugisha Mahakama hivi sasa ina uwezo wa kusikiliza mashauri yote yanayoingia mahakamani ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.
‘‘Taarifa hii inaelezea hali ya ufunguaji na usikilizaji wa mashauri ya jinai kwa kipindi cha Januari hadi Julai Mosi, 2020 kwa Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya nchi nzima.“Kwa upande wa Mahakama ya Rufani Tanzania, jumla ya mashauri ya jinai 297 yalifunguliwa na mashauri 210 yalisikilizwa sawa na asilimia 70.7 ya mashauri yote yaliyofunguliwa katika kipindi hicho,’’ alisema Kamugisha huku akisema wastani wa mzigo wa mashauri ni 737 kwa jopo la majaji wa tatu.
Alisema Mahakama Kuu ya Tanzania, mashauri ya jinai 2,561 yalifunguliwa na 2,618 yalisikilizwa sawa na asilimia 102.2. Wastani wa mzigo wa mashauri ni 345 kwa kila Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Kamugisha alisema katika Mahakama za Hakimu Mkazi jumla ya mashauri 5,338 yalifunguliwa, 5,566 yalisikilizwa sawa na asilimia 104.3 ya mashauri ya jinai yaliyofunguliwa. Hivyo wastani wa mzigo wa mashauri ni 198 kwa kila Hakimu.
“Mahakama za Wilaya mashauri 16,169 yalifunguliwa, mashauri 17,254 yalisikilizwa sawa na asilimia 97.5.Hadi kufikia Julai Mosi, 2020 wastani wa mzigo wa mashauri kwa Mahakama za Wilaya ni 96 kwa kila Hakimu,”alisisitiza
.
Aliongeza kwamba mashauri 333 yalifungiliwa katika Mahakama za Watoto, 302 yalisikilizwa sawa na asilimia 90.6.
Kwa upande wa ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, ambayo imewakilishwa na Naibu Kamishna wa Polisi Bw.Saleh Ambika alieleza kuwa lengo kuu la ofisi yake ni kuhakikisha upelelezi wa makosa ya jinai unafanyika na unakamilika kwa haraka zaidi kadri iwezekanavyo.
“Upelelezi wa makosa ya jinai una hatua mbalimbali na unahusisha taasisi mbalimbali za mfumo wa haki jinai kuna wakati mwingine Polisi wanahitaji kupata ripoti zinazotoka mamlaka nyingine kukamilisha upelelezi ili kumfikisha mtuhumiwa mahakamani kwa wakati,” alisema Ambika.
Alifafanua kuwa upelelezi unaohusisha sampuli za kitu fulani, Kitengo cha Upelelezi lazima kishirikiane na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali wakatiKmwingine sio rahisi kupata ripoti kwa kadri ya matarajio ya upelelezi wako, pia taasisi hiyo inataratibu zake za kiuchunguzi ili kukamilisha hilo,
Ambike alisema ushirikiano wadau hao upo kwa kiwango cha kutosha, hivyo hilo ndio lengo la kamati hiyo ni kuisaidia Mahakama ya Tanzania kufikia ajenda ya kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani.
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Huduma za Uangalizi kwa wafungwa wanaotumikia vifungo vya nje ya Magereza, Bw. Charles Nganze alisema wafungwa 706 walitumikia adhabu mbadala ya kufanya usafi wa mazingira kwenye maeneo ya Makaburi ya Kinondoni, mabwawa ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) , wizara na zahanati mbalimbali.
Naye Kamishna Msaidizi wa Magereza, Bw,Willington Kamuhuza, alishukuru jitihada zilizofanywa na wadau hao zimesaidia kupunguza msongamano wafungwa kwa asilimia 0.73.Pia aliongeza kwamba kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) jumla ya mikoa 16 iliyo na magereza mashauri hayo yamesikilizwa kwa njia ya Mahakama Mtandao baada ya kuwezeshwa kuwa na vifaa vya TEHAMA kutoka Mahakama ya Tanzania.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Uondoshaji wa Mashauri ya Jinai, ambaye pia ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt alisema lengo kikao hicho ni kutathmini utendaji kazi na kupanga mikakati ya kupunguza mlundikano wa mashauri ya aina hiyo.