Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART Mhandisi Ronald Lwakatare (katikati) akitoa maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha mabasi Gerezani kwa wakurugenzi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI walipokua katika ziara ya kukagua Awamu ya pili ya mradi wa BRT Juni 2, 2020.
***********************************
Na.Mwandishi Wetu
Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wamepongeza Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), kwa kasi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara ya Mabasi Yaendayo Haraka BRT awamu ya pili unaoendelea kutoka Gerezani Kariakoo kuelekea Mbagala.
Wakizungumza katika ziara ya kukagua miundombinu hiyo, Mkurugenzi wa Utawala na rasilimali Watu Bw. Victor Kategere na Mkurugenzi wa Manunuzi Bw. Lucas Suka wamesema kazi nzuri inayoendelea kufanyika inaridhisha na itakapokamilika wakazi wa Mbagala na maeneo ya jirani watafaidika na huduma za mabasi yaendayo haraka hivyo kuharakisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa ujumla.
Kwa upande wake Bw. Suka amesema, Serikali ina matarajio makubwa sana na Wakala katika kusimammia ujenzi huo ili ukamilike kwa wakati na kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha (value for money), pamoja na ubora wa hali ya juu.
“Binafsi naiona Dar es Salaam ambayo katika miaka michache ijayo haitakuwa kabisa na foleni, na kwa wakazi wa Mbagala uwepo wa miundombinu ya DART utawasaidia kuinua shughuli zao za kibiashara kwani wakazi wengi wa maeneo hayo ni wafanyabiashara na wajasiriamali wanaotegemea kupata bidhaa kutoka katika soko la Kariakoo na wengine kutoka soko kuu la samaki la Feri” Alisema Bw.Suka.
Akizungumza katika ziara hiyo Mtendaji Mkuu wa DART Mhandisi Ronald Lwakatare, amesema wakala umejipanga kuhakikisha awamu zote za ujenzi wa mradi zinakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa na wataendelea kuwa wabunifu kwa ajili ya kupata matokeo mazuri zaidi.
Kituo kikuu cha Mabasi Yaendayo Haraka cha Gerezani eneo la Kariakoo awamu ya pili kitakachohudumia mabasi yatakayotumia barabara ya Kilwa , ujenzi wake umefikia asilimia 76 na kazi inaendelea vizuri na hakuna tatizo lolote.
“Kituo cha Gerezani kwa ajili ya kupokea mabasi kutoka njia ya Mbagala awali kilisanifiwa kuwa na uwezo wa kupokea mabasi sita tu kwa wakati mmoja lakini baada ya kukaa na wataalam wangu tulikisanifu upya na kukijenga kivingine ambapo kitakuwa na uwezo wa kuchukua mabasi 24 kwa wakati mmoja katika kituo hicho bila kuongeza ukubwa wa eneo” Alisema Mhandisi Lwakatare.
Ujenzi wa mtandao wa barabara za Mabasi Yaendayo Haraka kuanzia Kariakoo kwenda Mbagala unahusisha pia Ujenzi wa vituo vya Gerezani pamoja na vituo vidogovidogo vya katikati, pia utahusisha ujenzi wa kituo kikubwa cha Mbagala kitakachojumuisha maegesho ya mabasi, majengo ya huduma za kiutawala, maegesho ya magari binafsi, huduma za kuosha magari na sehemu za kupumzikia abiria.
Ziara ya wakurugenzi hao katika miundombinu ya DART ni katika kutembelea na kukagua utekelezaji wa majukumu ya taasisi zilizoko chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI.