***********************************
Na Farida Saidy,Morogoro.
Watanzania waliobahatika kapata ajira katika mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere Mw2115 wametakiwa kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa juhudi kubwa ili kufanikisha azma ya serikali ya kukamilisha mradi huo ifikapo juni 2022.
Ameyasema hayo Naibu Waziri wa Nishati Mhe.Subira Mgalu mara baada ya kutembelea na kujionea kazi zinazofanywa na mkandarasi wa Mradi huo chini ya usimamizi wa shirika la umeme Tanzania TANESCO,ambapo amesema Serikali imeamua kujenga mradi wa Bwawa la NyerereMw 2115 kwa lengo la kuwapunguzia watanzania gharama za maisha hususani katika upatikanaji wa Umeme wa uhakika na wenye gharama nafuu.
Aidha Naibu Waziri Mgalu ameongeza kuwa kukamilika kwa Mradi wa Bwawa hilo kutasaidia upatikanaji wa Maji ya uhakika kwa matumizi ya Binaadamu,ambayo yatawasaidia katika shughuri za Kilimo Cha Umwagiliaji,Uvuvi pamoja na utalii,ambapo watajiongezee kipato Chao na taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine amesema amefurahishwa na tamko la Benki ya Dunia la kuitangaza Tanzania kufikia katika uchumi wa Kati na kukamilika kwa Mradi wa Bwawa la Nyerere Mw2115,kutaifanya Nchi kutoa ajira nyingi kwenye Sekta zilizo lasmi na zisizo rasmi,hivyo kutaifanya Tanzania kufikia katika uchumi wa Juu zaidi.
Kwa upande wake Naibu waziri wa viwanda na biashara Mhandisi STELLA MANYANYA amesema serikali itafuatilia wamiliki wote wa viwanda waliopewa tenda ya kusambaza vifaa vya ujenzi katika mradi wa Bwawa la kufua umeme la mwalimu Julius NyerereMw2115 ili kuhakikisha wanazalisha vifaa vitakavyokidhi ubora wa kazi hiyo inayogharimu fedha nyingi za serikali.
Nae Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji TANESCO Mhandisi Khalid James amesema wao kama wasimamizi wakuu wa mradi huo watahakikisha wanamsimamia vizuri mkandarasi katika kila hatua atakayofikia ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na uboara uliokusudiwa.
Pia Kaimu Mkurugenzi huyo amesema kuwa mpaka sasa mkandarasi amefikia asilimia 84 ya mpango kazi,ambapo kazi bado zinaendelea katika kujenga Handaki la kuchepusha Maji,kusaga mawe na kutengeneza zege na sehemu yanapohifandhiwa maji.
Katika ziara hiyo Naibu waziri wa Nishati Mhe Subira Mgalu aliambatana na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Muhandisi Stella Manyanya na Kaimu mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO Muhandisi Khalid James,ambapo wote kwa pamoja wamelidhishwa na kazi inayofanywa na mkandarasi.