Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Maonyesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam , Barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam, Julai 3, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
DAR ES SALAAM
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Serikali kupitia mpango wa maboresho ya mazingira ya biashara nchini (Blue Print) imeweza kufuta tozo 163 kati ya 173 zilizokuwa zikisababisha kero na usumbufu kwa wafanyabiashara nchini.
Akizungumza katika ufunguzi wa Maonyesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DIFT) leo Ijumaa (Julai 3, 2020), Waziri Mkuu Majaliwa alisema jitihada hizo za Serikali zinalenga kukuza mchango wa sekta ya biashara katika pato la taifa nchini.
Majaliwa alisema kupitia maboresho ya Blue Print, kati ya tozo hizo tozo 114 ni za sekta ya kilimo na mifugo, tozo 5 kutoka Wakala wa Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) na tozo 44 kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambazo zililalamikiwa na wafanyabiashara kutokana na kutoza gharama kubwa wakati wa uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
‘’Kufutwa kwa tozo hizo kumewezesha ongezeko la usajili wa taasisi ya OSHA kwa nafasi 16657 mwaka 2019 ikilinganishwa na nafasi 11663 mwaka 2018, hivyo Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya biashara nchini kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutunga Sheria za Uwezeshaji Biashara’’ alisema Majaliwa.
Kwa mujibu wa Majaliwa alisema Serikali pia inaendelea kupitia majukumu ya mamlaka mbalimbali za udhibiti ili kuhakikisha zinawawiana kimajukumu hatua inayolenga kuwaondolea usumbufu wafanyabiashara pindi wanapohitaji huduma mbalimbali zinazotolewa na mamlaka hizo.
Aidha Waziri Mkuu alisema kuwa Serikali pia itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara kwa kuweka mazingira bora na rafiki ili kuziwezesha sekta za viwanda na biashara kuendelea kuvutia wawekezaji na kuchangia katika ukuzaji wa uchumi wa nchi.
Aliongeza kuwa maonesho ya mwaka ya 2020, yamewekwa kimkakati ili kuwezesha shughuli za mazao, biashara pamoja na huduma kuweza kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi, hatua inayolenga kuziwesha sekta za kilimo, biashara kuweza kujitosheleza na mahitaji ya bidhaa muhimu ikiwemo chakula.
Akizungumzia taarifa ya hivi karibuni iliyotolewa na Benki ya Dunia, kuitangaza Tanzania kuingia katika nchi ya kipato cha kati, Majaliwa alisema juhudi hizo zimetokana na msukumo uliowekwa na Rais Dkt. John Magufuli wa kujenga sera imara za uchumi usio na utegemezi.
‘Mafanikio haya yanaiweka Tanzania katika ramani ya dunia, jambo kubwa ni kuwa tumeingia katika nchi ya kipato cha kati miaka 5 kabla ya malengo tuliyojiwekea katika kuifikia hatua hiyo mwaka 2025’’ alisema Majaliwa.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa alisema maonyesho ya mwaka 2020 yamepata mafanikio makubwa licha ya kuwepo tishio kwa tishio la ugonjwa wa COVID 19 kwani jumla ya washiriki 2880 wameshiriki maonyesho hayo wakiwemo washiriki wa ndani 2837 na washiriki 43 kutoka nje ya nchi.
Bashungwa alisema katika kuwezesha sekta za viwanda na biashara zinaendelea kupiga hatua nchini, Serikali imeendelea kuzihamasisha taasisi za kifedha ikiwemo mabenki na kutoa mikopo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wanaojitokeza kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogo katika maeneo mbalimbali nchini.
‘Tuna mkakati tuliojiwekea baina ya taasisi yetu ya SIDO na Benki ya Azania ya kupeleka mitaa ya SIDO Mikoani kwa ajili na taasisi zote za kifedha zikiiga mfano huu itakuwa rahisi kuwatambua wajasiriamali hao na kuweza kuwapa mikopo inayostahili’’ alisema Bashungwa.
Aidha Bashungwa alisema katika kipindi cha miaka mitano ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano jumla ya 8477, vilimeanzishwa ambapo jumla ya ajira 482,601 zimeweza kutolewa kwa watu mbalimbali.
‘’Wakati wa Janga la COVID, Sisi Tanzania kupitia viwanda vyetu vya ndani tuliweza kuzalisha barakoa na vitakasa mikono kwa kuwa kwani kila nchi ilizalisha bidhaa hizo kwa mahitaji yake, tunampongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa maono ya ujenzi wa viwanda ambapo leo yametuvusha katika janga la COVID-19 kupitia vifaa vilivyozalishwa na viwanda vyetu’’ alisema Bashungwa.
Kauli mbiu ya Maonyesho ya 44 ni ‘Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu’’.