Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimkabidhi hati ya kiwanja Bi. Zainab Selema Ketuba mwenye miaka 77 hati ya kiwanja ambacho amesema alinyanganywa tangu enzi za vita ya Idd Amin leo wakati wa uzinduzi wa Ofisi za Ardhi Mkoa wa Shinyanga
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack ramani ya eneo la utawala la Mkoa wa Shinyanga leo wakati wa uzinduzi wa Ofisi za Ardhi Mkoa wa Shinyanga.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akikata utepe kufungua rasmi ofisi za Ardhi Mkoa wa Shinyanga pamoja naye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack pamoja na Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Shinyanga leo wakati wa uzinduzi wa Ofisi za Ardhi Mkoa wa Shinyanga.
……………………………………………………………………
Anthony Ishengoma – Shinyanga
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi leo ametoa hati ya kiwanja kwa bibi wa miaka 77 ambaye amekuwa akikosa haki hiyo tangu mwaka 78 na kwa kumbukumbu zake ilikuwa tangu ya vita vya Kagera.
Akiongea mbele ya Waziri Lukuvi Bibi huyo wa miaka 77 Bi.Zainab Seleman Ketuba amesema alinyanganywa kiwanja chake tangu enzi za vita vya Idd Amini na hali hiyo ilijitokeza aliposafiri kwenda kushiriki Msiba wa Baba yake.
Lukuvi ametoa hati hiyo kwa bibi huyo pamoja na watu wengine leo wakati wa zoezi la uzinduzi wa Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Shinyanga na kusema kuwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga ambao wamekuwa wakifuatilia hati zao Mkoa wa Simiyu na Tabora sasa wataanza kufuatilia huduma za ardhi katika Ofisi mpya za ardhi zilizozinduliwa leo Mkoani Shinyanga.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema mkoa wa Shinyanga una zaidi ya Wananchi elfu 65 ambao michoro ya ramani na hati za viwanja vyao vimeidhinishwa lakini hawajafutilia katika ofisi za Ardhi za Wilaya ili wapatiwe hati na kuanza kulipa kodi ya ardhi na kuwataka kufanya hivyo ndani Siku 90.
Waziri lukuvi ameongeza kuwa Tanzania nzima ina watu takribani laki 9 ambao michoro ya ramani ya viwanja vyao tayari imeidhinishwa lakini hawajafika katika ofisi husika kulipia na kuchukua hati za viwanja vyao na kuongeza kuwa endapo watafuatilia na kuchukua hati zao na kulipa kodi ya ardhi Nchi itapata kiasi cha Sh. Bilioni 125.
Alibainisha kuwa mwananchi ambaye atashindwa kufuatilia hati yake katika kipindi cha siku tisini atapelekewa stakabadhi ya malipo alipe kuanzia tangu pale kiwanja chake kilipopimwa na michoro yake kuidhinishwa.
” Wale wamiliki ambao watashindwa kufuatilia hati katika kipindi cha siku 90 wataanza kudaiwa kodi ya pango la ardhi kuanzia pale ambapo kodi iliidhinishwa hata kama michoro hiyo ni ya tangu mwaka 1962 ataanza kuanzia hapo maana itakuwa ni uzembe.’’ Aliongeza Mhe. Lukuvi.
Waziri Lukuvi ameendelea kusema kuwa Serikali inataka kila mtanzania apate hati milki ya ardhi kwa mujibu wa sheria kwa kuwa Serikali haikusanyi kodi ya ardhi kwa mtu ambaye hana hati na kuwataka wachukue hati zao ili Serikali ipate mapato na kutoa huduma katika sekta za Barbara na hospitali.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack amesema kuanzishwa kwa ofisi ya ardhi Mkoa wa Shinyanga tayari ameanza kuona kupungua kwa migogoro ya ardhi Mkoani kwake.
“Kama Mkoa tutahakikisha tunaleta utulivu na kutokana na kuanzishwa kwa ofisi za ardhi katika Mkoa wa Shinyanga kwa kuwa migogoro itakuwa imepungua” Alisema Bi. Telack Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Tayari zoezi la uzinduzi wa ofisi za ardhi mikoa mbalimbali limefanyika katika mikoa kumi hapa Nchini na zoezi kama ili linaendelea katika mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Mwanza, Mara, Geita na Mkoa wa Kagera.