……………………………………………………………..
MKUU wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Deo Ndejembi ameagiza Wakala wa Misitu (TFS) wilayani humo kushirikiana na wenzao wa Wilaya ya Kiteto kuhakikisha wanatokomeza uharibifu wa mazingira katika Kata ya Njoge iliyopo mpakani mwa wilaya hizo mbili.
DC Ndejembi ametoa agizo hilo katika mkutano wa hadhara na wanakijiji wa eneo hilo ambapo ameagiza yoyote atakaekutwa akichunga mifugo au kufanya kilimo kwenye maeneo ya hifadhi kuchukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumza katika mkutano huo, DC Ndejembi amesema suala la utunzaji mazingira ni la lazima kwa sababu linahusu uhai wa kila mwananchi.
Amewataka TFS kutoa elimu ya uhifadhi mazingira kwa wananchi wilayani Kongwa na pia kuunda kamati ya mazingira itakayokua na kazi ya kusimamia utunzaji wa mazingira kwenye maeneo ya hifadhi.
” Ndugu zangu uharibifu wa mazingira ndio unaochangia hata kukosekana kwa mvua kwenye maeneo yetu lakini pia kunaua vyanzo vya maji, ndio maana hapa kila tukileta wachimbaji wa maji wanagundua maji yapo chini sana kwa sababu ya uharibifu wa mazingira.
Nitoa maagizo kwa TFS kusimamia utunzaji wa hifadhi kutoa elimu kwa wananchi na yeyote ambaye atakutwa anachunga mifugo yake au kufanya kilimo kwenye maeneo ya hifadhi achukuliwe hatua za kisheria,” Amesema DC Ndejembi.
Katika mkutano huo pia, DC Ndejembi amempongeza Rais Dk John Magufuli kwa kutekeleza ahadi yake ya kuinyanyua kiuchumi Tanzania baada ya kufanikisha kufikia uchumi wa kati ndani ya kipindi cha miaka mitano.
” Ndugu zangu wa Kongwa tuna kila sababu ya kumpatia kura nyingi sana Rais wetu katika uchaguzi mkuu unaokuja, kwa sababu alituahidi kuifanya Nchi yetu kuwa Nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025 lakini matokeo yake tumefikia lengo mwaka huu, haya ni mafanikio makubwa sana.
Rais wetu amefanya mengi makubwa, ujenzi wa Reli ya Kisasa, Ujenzi wa Bwawa la Umeme la Mwl Nyerere, kusambaza umeme kila Kijiji (REA), Elimu bila malipo na miradi mingine mikubwa nchini imesababisha kutuinua kama Taifa kufikia uchumi wa kati,” Amesema DC Ndejembi.
Kwa upande wake Meneja wa TFS, Wilaya ya Kiteto, Elias Sweti ameahidi kushirikiana na wenzake wa Kongwa kutoa elimu ya utunzaji wa hifadhi na mazingira kwa wananchi wa mpakani mwa wilaya hizo sambamba na kuunda kamati ya mazingira itakayoshirikisha wananchi wenyewe.